Hali inayoendelea Gaza na Ukingo wa Magharibi ni "ajabu" na "hatari sana," ujumbe wa Uturuki kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) umesema.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Ahmet Yildiz aliwasilisha taarifa ya mdomo ya Uturuki siku ya Jumatatu katika mashauriano kuhusu matokeo ya kisheria ya sera na mazoea ya Israel katika eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu ikiwemo Jerusalem Mashariki.
Yildiz alitoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano huko Gaza na mtiririko usiozuiliwa wa misaada kwa Wapalestina huku mwezi mtukufu wa Ramadhani unapokaribia.
"Inatisha kuona ripoti kuhusu mipango ya serikali ya Israel ya kuweka kikomo kwa maombi ya Waislamu katika Haram al Sharif wakati wa Ramadhani," alisema wakati wa mikutano ya hadhara huko The Hague, na kuongeza kwamba "maneno ya uchochezi" ya baadhi ya mawaziri wa Israel pia "ni ya kutisha."
Akielezea msimamo wa Ankara kuhusu hali ya Maeneo ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu, ikiwemo Jerusalem Mashariki, Yildiz alisema Uturuki "ina wasiwasi mkubwa" na sera na mazoea ya upande mmoja ya Israel, ambayo "yanakiuka hadhi ya Haram al Sharif."
Pia alibainisha kuwa hali inayoendelea tangu Oktoba 7 "kwa mara nyingine tena inathibitisha" kwamba hakuwezi kuwa na amani katika eneo hilo bila kushughulikia sababu kuu ya mzozo wa Gaza.
Mauaji ya kimbari na uhalifu wa kivita
Israel inashutumiwa kwa mauaji ya halaiki katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki.
Uamuzi wa muda wa mwezi Januari uliiamuru Tel Aviv kusitisha vitendo vya mauaji ya halaiki na kuchukua hatua za kuhakikisha kwamba misaada ya kibinadamu inatolewa kwa raia huko Gaza.
Israel ilifanya mashambulizi makali dhidi ya Gaza kufuatia shambulio la Hamas mnamo Oktoba 7.
Mashambulio ya mabomu ya Israel yameua zaidi ya watu 29,000 na kujeruhi zaidi ya 69,000 kwa uharibifu miundombinu na kusababisha uhaba mkubwa wa mahitaji.
Vita vya Israel dhidi ya Gaza vimesababisha asilimia 85 ya wakazi wa eneo hilo kuwa wakimbizi wa ndani huku kukiwa na uhaba mkubwa wa chakula, maji safi na dawa, wakati asilimia 60 ya miundombinu ya eneo hilo imeharibiwa, kulingana na Umoja wa Mataifa.