Wito wa viongozi wa mapinduzi ya Niger kwa kipindi cha mpito cha miaka mitatu kurudisha demokrasia "haukubaliki", mwakilishi wa jumuiya ya Afrika Magharibi, ECOWAS, amesema.
"Mabadiliko ya miaka mitatu hayakubaliki," Abdel-Fatau Musah, kamishna wa siasa na usalama wa ECOWAS, aliiambia idhaa ya Al Jazeera katika matangazo ya mahojiano siku ya Jumatatu.
"Tunataka utaratibu wa kikatiba urejeshwe haraka iwezekanavyo."
Katika hotuba yake kwa njia ya televisheni siku ya Jumamosi, Jenerali Abdourahamane Tchiani wa Niger alisema muda wa mpito wa mamlaka hautazidi miaka mitatu, baada ya maafisa wa jeshi kumuondoa madarakani Rais Mohamed Bazoum mnamo Julai 26.
Tchiani alizungumza baada ya ujumbe kutoka Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) kuitembelea Niger kwa msukumo wa mwisho wa kidiplomasia kabla ya kuamua kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya watawala wapya wa Niger.
Aliishutumu ECOWAS kwa kujiandaa kushambulia Niger kwa kuanzisha kikosi cha kuvamia kwa ushirikiano na jeshi la kigeni, bila kutaja nchi gani.
Lakini viongozi wa ECOWAS wanasema wanapaswa kuchukua hatua kwa kuwa Niger imekuwa taifa la nne la Afrika Magharibi tangu 2020 kukumbwa na mapinduzi, kufuatia Burkina Faso, Guinea na Mali.