Ghetto Kids wa Uganda Wavutia Majaji wa Uingereza, wapokea sifa adimu

Ghetto Kids wa Uganda Wavutia Majaji wa Uingereza, wapokea sifa adimu

Wapokea ishara kwa njia ya "Golden Buzzer" kuonyesha kwamba wanakubalika na majaji bila pingamizi
Ghetto Kids | Picha: Britains Got Talent

Wasanii wengi wazuri walipanda jukwaani kupigania tuzo kuu ya kipindi cha Britain’s Got Talent iliporejea kwenye televisheni jana usiku.

The Royal Variety Performance, tukio la kila mwaka la televisheni linalofanyika nchini Uingereza ili kuchangisha fedha kwa ajili ya Shirika la Msaada la Royal Variety pamoja na pesa za zawadi, huvutia kila mtu kuanzia wacheza densi na waimbaji hadi wachekeshaji na wana mazingaombwe kwa matumaini ya kuwavutia majaji na kupata nafasi mwaka huu katika raundi ya nusu fainali.

Kikundi cha densi kutoka Uganda kiitwayo Ghetto Kids, kinachoundwa na watoto 30 wanaoishi katika kituo cha kulelea watoto yatima, kilijishindia nafasi ya moja kwa moja ya kuongia kwenye nusu fainali kwa kupata "Golden Buzzer" kwa onyesho lao la kusisimua na kufurahisha katika kipindi cha vipaji maarufu ya Britains Got Talent.

"Golden buzzer" ni kitufe kinabonyezwa kushinikizwa na jaji kwamba wanataka mshiriki apite moja kwa moja mpaka kwenye vipindi vya mubashara bila kupingwa. Kupata Golden Buzzer sio kitu cha kawaida.

Katika video iliyotumwa Facebook, Bruno Tunioli, ambaye ni jaji wa muziki wa densi, alifurahishwa sana na uchezaji wao wa ajabu kiasi kwamba, katikati ya maonesho, alishindwa kujizuia na kubonyeza kitufe cha dhahabu. Kitu kilichowashangaza wengi.

Licha ya kuwa na furaha tele, kikundi hicho cha watoto wa Uganda kiliendelea na maonyesho.

Jaji mwingine, Simon Cowell alisema kuwa hii "haijawahi kutokea" hapo awali huku wasikilizaji na majaji wengine wakishangaa kwa kutoamini.

"Nyinyi ni nyota wanaong’aa, tunafurahi sana kuwa nanyi katika onyesho la Britain’s Got Talent." Alisema jaji Alesha Dixon.

Wakati huo Josephine mwenye umri wa miaka mitano alipojiunga na kikundi kwenye jukwaa, majaji walitazama kwa mshangao mkubwa huku umati ukimshangilia kwa hatua jinsi anavyocheza kwa step bila kosa.

Daouda Kavuma, ambaye alianzisha shirika hilo mwaka 2014 linaloundwa na watoto kutoka makazi duni ya Katwe huko Kampala, Uganda, hakuweza kuzuia furaha yake pia.

TRT Afrika