Ghetto Kids

Iwapo kuna wakati mzuri zaidi wa muujiza, basi ni sasa baada ya kundi la wachezaji wachanga wa Uganda kunusia ushindi baada ya kutinga fainali ya onyesho maarufu la talanta la Uingereza, Britain Got Talent.

Wachezaji hao, ni baadhi ya familia ya watoto 30 waliolelewa na Kavuma Dauda. Shule yake imetoa makazi, chakula, na elimu kwa watoto katika mitaa ya Kampala tangu 2007.

‘’Tunawashukuru mashabiki wetu kwa kutuunga mkono. Tutaendelea kutumia muziki kusaidia watoto yatima na wasiojiweza. Asante kwa mashabiki kwa kutupenda," Dauda aliiambia TRT Afrika.

Kikundi hiki cha densi cha Ghetto Kids walipata umaarufu zaidi kwenye mitandao ya kijamii mwezi uliopita baada ya kujishindia nafasi ya moja kwa moja ya kuingia kwenye nusu fainali kwa kupata "Golden Buzzer" kwa onyesho lao la kusisimua na kumfanya jaji Bruno Tunioli kushindwa kujizuia na kubonyeza kitufe hicho.

Kupata Golden Buzzer sio kitu cha kawaida . Inamaanisha kuruka hatua ya bootcamp, ambapo nafasi zinashindaniwa vikali."Golden buzzer" ni kitufe kinabonyezwa kushinikizwa na jaji kwamba wanataka mshiriki apite moja kwa moja mpaka kwenye vipindi vya mubashara bila kupingwa.

Ghetto Kids ilivutia hadhira ya kimataifa, na video yao ya majaribio ya Golden Buzzer ikipata kutazamwa zaidi ya mara milioni 1.2 kwenye YouTube. Walikuwa wa kwanza kupata mafanikio haya katika onyesho la mwaka huu.

Jumapili usiku, wana jukumu la kuiba mioyo ya watazamaji tena, wakicheza katika fainali kali ambayo inaangazia talanta zingine za kipekee.

Kutwaa hii kutawahakikishia wachezaji wachanga zawadi ya £250,000 pesa taslimu pamoja na ridhaa na manufaa mengine.

Nnchini kwao, Uganda, mashabiki wanawapigia debe na kuungwa mkono hasa kwenye mitandao ya kijamii.

Ghetto Kids watachuana uso kwa uso dhidi ya waimbaji Travis George, Olivia Lyner, na Malakai Bayoh; wachezaji Lilliana Clifton na Musa Motha, mcheshi Viggo Venn, mchawi Cillian O’Connor, na wanasarakasi Duo Odyssey

TRT Afrika