Magari yaliharibiwa na mashabiki waliokuwa na hasira baada ya Côte d'Ivoire kupoteza 4-0 dhidi ya Equatorial Guinea kwenye AFCON 2023 Januari 22, 2024. / Picha: TRT Afrika

Ghasia zilizuka mjini Abidjan, Côte d'Ivoire baada ya wenyeji wa AFCON 2023 kuchapwa 4-0 na Equatorial Guinea katika mechi ya mwisho ya Kundi A Jumatatu.

Maelfu ya mashabiki waliondoka kwenye Uwanja wa Alassane Ouattara kabla ya kipenga cha mwisho.

Baadhi ya mashabiki wa Côte d'Ivoire waliokata tamaa waliharibu magari na kuvunja vioo vya mabasi, waandishi wa TRT Afrika walishuhudia.

Haijabainika mara moja iwapo kulikuwa na majeraha au vifo kufuatia ghasia hizo.

Usalama wa wachezaji

Mashabiki wachache walipambana na wasimamizi uwanjani, huku chupa za maji na viti vikirushwa uwanjani.

Wachezaji wa timu ya taifa ya Côte d'Ivoire walilazimika kusindikizwa hadi kwenye vyumba vyao vya kubadilishia nguo chini ya ulinzi mkali.

Wenyeji wako katika nafasi ya tatu ya kundi hilo wakiwa na alama tatu, na sasa wanatumai kuwa alama zao tatu zitatosha kumaliza kati ya washindi wanne bora waliomaliza nafasi ya tatu, ambao pia wamefuzu kwa 16 bora.

Equatorial Guinea inaongoza Kundi A ikiwa na pointi saba na tofauti kubwa ya mabao, mbele ya Nigeria iliyo nafasi ya pili, ambayo pia ina pointi saba.

Bao la kujifunga la Emilio Nsue

Guinea-Bissau walio pia kwenye kundi hilo, walimaliza mbio zao katika mchuano huo wakiwa na alama sifuri kutoka kwa mechi tatu.

Emilio Nsue alifunga mabao mawili Equatorial Guinea ilipoilaza Côte d'Ivoire 4-0 siku ya Jumatatu. Pablo Ganet na Jannick Buyla walikuwa wafungaji wengine wa Equatorial Guinea, ambao sasa wanafuzu hadi hatua ya 16 pamoja na Nigeria.

Côte d'Ivoire ilikumbana na kichapo kizito zaidi katika michuano ya AFCON siku ya Jumatatu, baada ya kushindwa 4-1 dhidi ya Ghana mwaka wa 1965, na kwa matokeo sawa na Misri mwaka wa 2008.

TRT Afrika