Mkutano kati ya viongozi wa Misri unakuja huku kukiwa na mvutano kuhusu mradi wa bwawa. Picha: Ethiopia PMO

Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed wametangaza hatua kubwa kuhusu mzozo ulioko baina yao juu ya bwawa la Ethiopia.

Katika taarifa ya pamoja nchi hizi mbili, zimekubaliana kuharakisha mashauriano ya kupata makubaliano kati ya Misri, Ethiopia na Sudan juu ya kulijaza bwawa la Ethiopia kwenye Mto Nile katika kipindi cha miezi minne.

Ndani ya muda huo, viongozi hawa wawili pia wamesema wataweka utaratibu wa utumiaji wa bwawa hilo.

Kwa upande wake Ethiopia imeashiria kujitolea katika kuhakikisha shughuli ya kulijaza bwawa lake mwaka huu , itazingatia maslahi ya Misri na Sudan kwa njia itakayohakikisha nchi zote zinapata mahitaji yake ya maji.

Walikuwa wakizungumza kando ya mkutano ulioandaliwa na Misri wa viongozi na majirani wa Sudan kujadili njia za kumaliza mzozo wa wiki 12 kati ya pande hasimu za kijeshi za Sudan ambao umesababisha janga kubwa la kibinadamu katika eneo hilo.

Utata wa bwawa

Misri na Ethiopia, majirani wawili wakubwa wa Sudan, zimekuwa katika mzozo katika miaka ya hivi karibuni kuhusu ujenzi wa bwawa kubwa Grand Ethiopian Renaissance (GERD) la kuzalisha umeme kwenye Blue Nile, karibu na mpaka na Sudan.

Misri inaiona GERD kama tishio lililopo kwa sehemu yake ya maji kutoka Nile na inataka Addis Ababa kufikia makubaliano ya lazima juu ya kujaza na uendeshaji wa bwawa hilo.

Ethiopia inaona bwawa hilo kama muhimu kwa mchakato wake wa maendeleo na inakanusha madhara yoyote kwa sehemu ya maji ya Misri na Sudan, nchi mbili za chini ya mto.

Mwezi Mei, mkutano wa nchi za kiarabu ulitoa azimio linalosisitiza kuunga mkono matakwa ya Misri ya kufikia makubaliano ya lazima na Ethiopia juu ya kujaza na uendeshaji wa GERD.

Haijabainika mara moja iwapo mazungumzo ya hivi punde kati ya viongozi wa Misri na Ethiopia yamezaa makubaliano au maazimio yoyote.

TRT Afrika