Jumuiya ya kanda ya Afrika Magharibi ECOWAS imeelezea "kuchukizwa" baada ya watu wasiojulikana kujaribu kuvamia kambi moja katika mji mkuu wa Sierra Leone, Freetown siku ya Jumapili.
Rais Julius Maada Bio alitaja tukio hilo "ukiukaji wa usalama" katika kambi ya Wilberforce.
Wanajeshi katika kambi hiyo walifanikiwa kuwafukuza wavamizi hao, Bio alisema katika taarifa yake kwenye mtandao wa kijamii wa X siku ya Jumapili.
Waziri wa Habari na Elimu ya Uraia wa Sierra Leone, Chernor Bah, alisema washukiwa hao hawakufanikiwa "jaribio la kuingia kwenye hifadhi ya kijeshi."
Amri ya kutotoka nje nchi nzima
"Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) imejifunza kwa kuchukizwa sana na njama ya baadhi ya watu kupata silaha na kuvuruga amani na utaratibu wa kikatiba nchini Sierra Leone," chombo hicho cha kikanda kilisema katika taarifa.
"ECOWAS inalaani kitendo hiki na inataka kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa washiriki wote katika kitendo hiki haramu. ECOWAS inasisitiza kutovumilia kwake mabadiliko ya serikali kinyume na katiba."
Kufuatia tukio la Jumapili, Rais Bio alitangaza amri ya kutotoka nje kwa muda usiojulikana nchini kote.
"Wananchi wanahimizwa kusalia majumbani," Bio alisema, akiongeza kuwa msako wa "mabaki ya waasi wanaokimbia" unaendelea.