Jumuiya ya kanda ya Afrika Magharibi ECOWAS imezitaka Burkina Faso, Mali na Niger kubatilisha uamuzi wao wa hivi majuzi ambapo kwa pamoja walitangaza kujiondoa kwenye chombo hicho.
Rais wa ECOWAS Omar Touray alisema Jumamosi kwamba iwapo mataifa yatajiondoa katika jumuiya ya kikanda, kutakuwa na "madhara ya kisiasa, kijamii, kiuchumi, kifedha na kitaasisi kwa nchi hizo tatu na pia kwa ECOWAS kama kanda."
Touray alizungumza baada ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) kufanya kikao kisichokuwa cha kawaida katika mji mkuu wa Nigeria Abuja kushughulikia "matukio makubwa" katika kanda na hali ya kisiasa nchini Burkina Faso, Mali na Niger.
Touray alitoa mfano wa mapambano dhidi ya ugaidi kama eneo ambalo nchi tatu wasio na uwezo wangeweza kukabiliana na changamoto kubwa iwapo wataondoka ECOWAS.
'Kuathiri ushirikiano wa usalama'
"... ndani ya mfumo wa ushirikiano wa kikanda dhidi ya ugaidi, itikadi kali na uhalifu uliopangwa, nchi hizo tatu zilinufaika kutokana na takriban dola milioni 100 zilizokusanywa katika muktadha wa mpango wa utekelezaji wa ECOWAS dhidi ya ugaidi," Touray alisema.
"Zaidi ya hayo, baadhi ya mgao wa fedha - kama dola milioni 7.5 - unafanywa kusaidia nchi hizo tatu katika kupata vifaa vya kusaidia vita vyao dhidi ya ugaidi.
"Kujiondoa kutaathiri ushirikiano wa kiusalama katika suala la kugawana taarifa za kijasusi na ushiriki katika mipango ya kikanda ya kukabiliana na ugaidi."
Touray aliendelea kusema kuwa Burkina Faso, Mali na Niger zinaweza kuteseka kutengwa kidiplomasia endapo wataondoka kwenye umoja wa kikanda.
'Kuchukua viza'
"Mamlaka inatambua kuwa uondoaji huo utaathiri moja kwa moja hali ya uhamiaji ya raia, kwani wanaweza kuhitajika kupata viza ya kuzunguka mkoa huo," alisema.
"Wananchi wanaweza kukosa tena kuishi au kuanzisha biashara chini ya mpangilio wa ECOWAS, na wanaweza kuwa chini ya sheria mbalimbali za kitaifa," Touray aliongeza, akisema kuwa nchi hizo tatu zinaweza kupoteza soko kubwa la ECOWAS.
Burkina Faso, Mali na Niger zinachukua zaidi ya 17% ya wakazi wa ECOWAS wa watu milioni 425.
Nchi hizo tatu, zilipokuwa zikitangaza kuondoka katika ECOWAS mwishoni mwa mwezi Januari, zilisema jumuiya ya kikanda ilizilenga kwa vikwazo vya "kinyama" vya kifedha na biashara.
'Kukuza umoja wa kikanda'
Siku ya Jumamosi, ECOWAS ilitangaza kuwa imeondoa vikwazo dhidi ya Guinea, Mali na Niger. Hali ya vikwazo ilivyowekewa Burkina Faso haikufahamika mara moja.
Touray alisema kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya Guinea, Mali na Niger kunalenga "kukuza umoja na usalama wa kikanda", na pia "kukuza biashara na manufaa yanayotokana na miradi na programu kadhaa za kikanda, ikiwa ni pamoja na Hifadhi ya Usalama wa Chakula ya Kanda."
ECOWAS ilisema iko tayari kufanya mazungumzo na Burkina Faso, Mali na Niger ili kufikia mwafaka.
Nchi hizo tatu zilikuwa zimewasilisha rasmi notisi zao za kujiondoa kwa mamlaka ya ECOWAS mwishoni mwa Januari.
Kutekeleza mabadiliko katika muda wa mwaka
Sasa bado haijafahamika iwapo Burkina Faso, Mali na Niger zingebatilisha uamuzi wao wa pamoja baada ya ECOWAS kuondoa vikwazo kwa baadhi yao.
Uondoaji wao uliopangwa kutoka kwa ECOWAS utaanza kutekelezwa katika muda wa mwaka mmoja kuanzia Januari 2024, kulingana na sheria za kambi hiyo ya kikanda.