Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) imeazimia kuweka vikwazo vya kifedha mara moja dhidi ya Niger baada ya wanajeshi kufanya mapinduzi dhidi ya Rais Mohamed Bazoum siku ya Jumatano.
Mji mkuu wa Nigeria, Abuja, ulikuwa mwenyeji wa mkutano maalum wa umoja huo kuhusu hali ya kisiasa nchini Niger siku ya Jumapili. Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat alikuwa miongoni mwa viongozi waliohudhuria.
Shirika la habari la AFP, likimnukuu afisa wa ECOWAS, lilisema vikwazo hivyo vitawekwa mara moja. Baadhi ya vikwazo ni pamoja na kufungwa kwa mipaka ya ECOWAS na Niger na kuweka marufuku ya kusafiri kwa wanajeshi walioasi.
Mwenyekiti wa ECOWAS, Bola Tinubu, ambaye pia ni Rais wa Nigeria, alisema jumuiya ya kikanda bado inamtambua Bazoum kama mkuu wa nchi wa Niger.
“Afrika imefikia kiwango ambapo 'Tunakataa mapinduzi,' kukatizwa kwa utaratibu wa kikatiba,” alisema katika hotuba yake wakati wa mkutano huo.
‘Lazima tuchukue hatua kali’
“Mmoja wetu, Bazoum, anashikiliwa mateka na jeshi lake. Hilo ni shambulio la kila mmoja wetu na lazima tuchukue hatua kali sana. Moja, kulinda maisha ya Rais Bazoum.'' amesema Tinubu. ''Kuvuruga utaratibu wa kidemokrasia kumesababisha watu wa Niger kuwa katika hali ya kutokuwa na uhakika na mazingira magumu,” Tinubu aliwaambia wakuu wenzake wa nchi za Afrika Magharibi.
"Nimewajulisha baadhi yenu kuhusu hatua ambazo tumechukua kukabiliana na shambulio hili na kuhakikisha kwamba mwenzetu, Rais Bazoum, yuko salama, na kwamba demokrasia inarejeshwa katika Jamhuri ya Niger. Ama tuite mazungumzo ya kujenga au kubomoa , chochote wewe na mimi tukisuluhisha kitatengeneza au kuharibu sifa zetu za kidemokrasia,” aliongeza.
"Nataka tuwe na nguvu, nguvu na uthabiti kuhusu kuendelea kuwepo kwa Bazoum pamoja na uhuru na urejesho wa chombo kilichochaguliwa kikatiba katika Jamhuri ya Niger. Hakuna wakati tena wa sisi kutuma ishara ya onyo, ni wakati wa kuchukua hatua na tunapaswa kuzungumza."
ECOWAS pia iliazimia "kutumia nguvu" ikiwa siku saba zitaisha wakati Bazoum bado yuko kizuizini.
Abdourahamane Tchiani, mkuu wa Walinzi wa Rais, kitengo kilichomuondoa Bazoum madarakani, amejitangaza kuwa rais wa mpito wa Niger.