Jopo la majaji wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ)./Picha: EACJ x.com

Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) sasa itasubiri maelezo ya kimaandishi ili iweze kuamua shauri linalopinga Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuwa sehemu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Hii ni baada ya chombo hicho, kinachoketi jijini Arusha, Tanzania kuhairisha shauri hilo hapo awali.

Hata hivyo, EACJ bado haijaweka wazi ni lini itatoa hukumu ya kesi hiyo.

Kupitia shauri namba 11 la mwaka 2020, raia wa Uganda Adam Kyomuhendo, anawashitaki wanasheria wakuu kutoka nchi za Uganda, Kenya, Tanzania, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na pia Katibu Mkuu wa Jumuiya ya EAC.

Katika hoja yake ya msingi, Kyomuhendo anasisitiza kuwa DRC haikuwa na sifa wala vigezo vya kujiunga na Jumuiya hiyo, kwa madai kwamba ilikiuka haki za kibinadamu.

Kyomuhendo anadai kuwa DRC ilishindwa kufikia vigezo vilivyoainishwa kwenye Vifungu 3(3) (a), (b) na (f) vya Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

DRC inatuhumiwa kwa kuwaweka vizuizini raia kadhaa wa Uganda, wakiwemo Samuel William Mugumya, Stephen Mugisha, Aggrey Kamukama, Joseph Kamugisha, Nathan Bright na wengine 35, katika gereza la kijeshi la Ndolo lililoko nchini DRC.

Kesi hiyo ilifunguliwa katika mahakama ya hiyo, Mei 4, 2020, kabla ya DRC kuwa mwanachama wa EAC.

DRC ilijiunga rasmi kama mwanachama wa saba wa EAC, mwezi Machi 2022.

TRT Afrika