Jumuiya ya Afrika Mashariki inatoa wito kwa pande zote husika kutekeleza usitishaji vita katika Mashariki ya DRC ili kuwezesha mazungumzo ya maana ya kumaliza mgogoro unaoendelea.
Rais William Ruto, ambaye ndiye mwenyekiti wa Jumuiya ya EAC, alisema katika htuba yake kuwa lazima pia makundi ya waasi yasitishe kusogeza mbele majeshi yao kuonesha nia safi katika mazungumzo hayo.
'Hasa ningependa kuwaomba wapiganaji wa M23 kusitisha kuvamia vijiji zaidi na miji na upande wa jeshi la kitaifa la DRC kusitisha hatua za kulipiza kisasi,'' alisema Rais Ruto.
Ruto aliongeza kuwa usitishwaji mapigano mara moja ndio nnjia pekee ya kuunda mazingira chanya ya kutafutia suluhisho mgogoro huo.
Aliongeza kuwa kama wanachama wa Jumuiya ya EAC na Umoja wa Mataifa, hawana budi kusimama kidete na kuheshimu sheria ya mipaka ya nchi na uhuru wa kujitawala na kuimarisha ujirani wema.
Rais Ruto alisisitiza pia umuhimu wa kulindwa na kuhifadhiwa wafanyakazi pammoja na mali za kidiplomasia zikiwemo mabalozi na mali zake pamoja na walinda amani waliotumwa katika nchi wanachama.
''Mazungumzo si ishara ya udhaifu bali ni ushahidi wa hekima na nguvu zetu zote kama viongozi na jumuiya,'' alisema Ruto katik ahotuba yake.
Tangu kuzuka mapigano yanayoongozwa na M23 katika Mashariki mwa DRC, kumekuwa na visa vya kuchomwa baadhi ya mabalozi katika mji mkuu Kinshasa huku waasi wakilaumiwa kwa mauaji ya walinda amani wa SADC wengi wao kutoka Afrika Kusini.
''Ni wazi kutokana na muingilio wa wahusika kutoka nje, kuwa mgogoro huu umechukua sura mpya na hauwezi kupuuzwa. Lazim atukubali kuwa huu mgogoro hauwezi kutatuliwa kwa nguvu ya kijeshi, bali kutumia diplomasia ya hali ya juu,'' aliongeza Rais Ruto.
Mwenyekiti wa SADC
Kwa upande wake Mwenyekiti wa SADC ambaye ndiye Rais wa Zimbabwe Emerson Mnangagwa alisisitiza haja ya kulinda raia katikati ya mapigano yanayoendelea Mashariki mwa DRC.
''Ujio wetu pamoja katika kikao hiki cha majumuiya mawili, ni ishara ya mshikamano na kujitolea kwetu kwa itikadi ya waanzailishi wa Umoja wa Afrika,'' alisema Rais Mnangagwa.
Aliendelea kusisitiza haja ya kufikiwa uamuzi thabiti na hatua za mara moja kuchukuliwa kuhakikisha amani Mashariki mwa Congo.
Aliwataka viongozi pia kutafuta hatua za dharura kuchukuliwa kuepuka janga la kibinadamu katika DRC.
Viongozi wa Mataifa ya EAC, walihudhuria binafsi akiwemo Rais wa Rwanda Paul Kagame, japo mwenzake wa DRC, Felix Chisekedi, alihudhuria kwa njia ya simu ya video kutoka sehemu nyingine.
Kwa sasa marais hao wameingi akikao cha faragha bila waandishi wa habari ili kujadiliana zaidi.
Mkutano unafanyika jijini Dar es Salaam kwa mualiko wa mwenyeji Rais Samia Suluhu Hassan.