Kiongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi amesema yuko tayari kwa mazungumzo na mwenzake wa Rwanda kwa ajili ya kutafuta amani lakini amelaani mkataba wa hivi karibuni kati ya Rwanda na Umoja unaohusiana na madini.
“Huu ni uchokozi,” alisema Rais Tshisekedi katika mahojiano ya ana kwa ana na waandishi wa habari wa Televisheni ya Taifa ya RTNC, siku ya Alhamisi.
Tshisekedi aliituhumu Rwanda kwa kuiibia nchi yake madini.
Pia alikosoa makubaliano ya hivi karibuni kati ya Rwanda na Umoja wa Ulaya, mwanzoni mwa wiki hii, unaolenga kuimarisha ushirikiano katika sekta ya madini, hususani kuhusu malighafi muhimu kama vile tantalum.
Rwanda haipaswi kuuza utajiri ambao sio wake, alisema.
Waasi wa M23
Tshisekedi anaamini kuwa mapato kupitia mauzo hayo haramu, yatawezesha kuimarisha majeshi yao na kuendelea na malengo yao nchini Congo.
Aliituhumu Rwanda kwa kukiunga mkono kikundi cha M23, kinachofanya mashambulizi ya mara kwa mara mashariki mwa Congo.
“Rwanda inaendelea kujificha nyuma ya kivuli cha M23, na ndio maana siko tayari kufanya mazungumzo na kikundi hichi cha magaidi,” alisema, wakati anajibu swali la iwapo yupo tayari kufanya mazungumzo na kikundi hicho.
“Kipaumbele changu ni amani, nataka amani ya kudumu kwa nchi yangu, kwa hilo niko tayari kuweka pembeni tamaa zangu za kivita. Kama sote tuko tayari bila vita, nami nitaafiki hilo kwa mikono miwili. Lakini kama litahitaji vita, nitafanya hivyo kwa mikono miwili pia,"aliongeza.
Tshisekedi analenga kukutana na mwenzake wa Angola Joao Lourenco mnamo Februari 27. Lourenco ni mpatanishi katika mgogoro huu.
Mara kadhaa, Rais wa Rwanda Paul Kagame amekana kuhusishwa na kukiunga mkono kikund cha waasi wa M23.