DRC inasema ndege za kiraia ziligongwa wakati wa shambulio la ndege isiyo na rubani. Picha: AFP

''Jeshi la Rwanda lilifanya shambulizi la "drone" kwenye uwanja wa ndege wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mashariki mwa Goma, ambalo liliharibu ndege za raia,'' jeshi la Congo lilisema Jumamosi.

Shutuma hizo zimekuja baada ya mlipuko wa bomu kuripotiwa mapema Jumamosi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Goma katika jimbo la Kivu Kaskazini huku kukiwa na mapigano yanayoendelea kati ya waasi wa M23 na vikosi vya serikali.

"Ndege zisizo na rubani za jeshi la Rwanda zililenga ndege za FARDC (jeshi la DR Congo), mwendo wa alfajiri Jumamosi," msemaji wa jeshi katika jimbo la Kivu Kaskazini, Guillaume Djike Kaïko, alisema katika video iliyosambazwa na mamlaka ya mkoa.

Lakini "ndege ya FARDC haikugongwa, bali ni ndege za kiraia ambazo ziliharibiwa," alisema.

Waasi waendelea kusonga mbele

Hali ya usalama bado ni tete karibu na Goma, ambako maelfu ya wakaazi wanaokimbia vita wametafuta usalama huku kukiwa na mapigano makali.

Hivi majuzi, ndege za kivita za Congo zimeripotiwa kutumika kuwashambulia waasi wa M23 baada ya mapigano kushika kasi karibu na mji wa kimkakati wa Sake, kilomita 20 kutoka mji mkuu wa mkoa, Goma.

Sake inasemekana kuwa kizuizi cha mwisho kabla ya Goma, ambayo kutekwa kwake na waasi kungekata mji huo.

Congo inaishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 wanaopambana na vikosi vya serikali mashariki mwa nchi, madai ambayo Kigali inakanusha mara kwa mara.

Kigali pia imeishutumu Kinshasa kwa kuchochea mapinduzi ya utawala nchini Rwanda.

Hakukuwa na jibu la mara moja kutoka kwa jeshi la Rwanda juu ya madai ya hivi karibuni.

Kikosi cha kikanda

Wakati huo huo, Rwanda iliomba Umoja wa Mataifa kutounga mkono kikosi cha kikanda kilichotumwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kupambana na makundi yenye silaha, ikitilia shaka kutoegemea upande wowote kwa tume hiyo.

Kikosi cha Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) "si jeshi lisiloegemea upande wowote katika mgogoro uliopo," Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Vincent Biruta alisema katika waraka uliotumwa kwa Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uliwekwa wazi siku ya Ijumaa.

Biruta alidai kuwa ujumbe wa SADC ulilenga "kuunga mkono mkao wa uhasama wa Serikali ya DRC, ambao una uwezekano wa kuongezeka zaidi kwa mzozo na kuongezeka kwa mvutano katika eneo hilo."

Rwanda haitakuwa na tatizo na Umoja wa Mataifa kusaidia vikosi vya kanda kama vina nia ya kweli kuleta amani katika eneo la mashariki la DRC lenye machafuko, aliongeza.

Juhudi za upatanishi

Haya yanajiri huku kukiwa na mapigano yanayoendelea kati ya waasi wa M23 na jeshi la Congo katika jimbo la Kivu Kaskazini mashariki mwa DRC, na kusababisha maelfu ya watu kuyahama makaazi yao.

Mwezi uliopita, jeshi la Kongo lilitangaza kuanza kwa mashambulizi ya pamoja na wanajeshi kutoka SADC mashariki mwa nchi hiyo, huku amri ya mashambulizi ikiwalenga zaidi waasi wa M23.

Siku ya Ijumaa, Rais wa Kongo Felix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda, Paul Kagame, walikutana Addis Ababa, Ethiopia katika mkutano mdogo ulioandaliwa na Rais wa Angola João Lour enço kujadili mzozo wa mashariki mwa Congo.

Raia waliokimbia makazi yao

Lourenco, mpatanishi mteule wa Umoja wa Afrika kuhusu hali ya amani na usalama mashariki mwa Kongo, alisisitiza haja ya kufufua mchakato wa amani na kufikia usitishaji mapigano kati ya wanajeshi wa Kongo na waasi wa M23, pamoja na kuanzisha mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Tshisekedi. na Kagame kumaliza mgogoro kati ya nchi hizo mbili jirani.

Tangu wiki ya kwanza ya Februari, takriban raia 15 wameuawa na 29 kujeruhiwa karibu na Goma na Sake, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) lilisema mapema wiki hii.

Takriban wakimbizi wa ndani 135,000 wamekimbia Sake hadi Goma, kulingana na UNHCR.

TRT Afrika