Na Ramadhan Kibuga
TRT Afrika, Bujumbura
Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo inasubiria hadi sasa matokeo ya Uchaguzi wa wabunge, wa wakuu wa majimbo pamoja na madiwani uliofanyika sambamba na uchaguzi wa Urais tarehe 20 Disemba.
Uchaguzi huo wa Urais kulingana na matokeo ya awali ulishuhudia ushindi wa Rais aliye madarakani Felix Tshisekedi kwa zaidi ya asilimia 73 ya kura.
Uchaguzi huo uligubikwa na dosari nyingi kulingana na waangalizi mbalimbali wa kura hiyo ambao waliichagiza Tume ya Uchaguzi kuchukua hatua. CENI ilitangaza msururu wa hatua ikiwemo maazimio mawili makubwa : Kwanza kufutilia mbali uchaguzi wa wabunge wa kitaifa na wabunge wa mkoa katika majimbo mawili: Masi-manimba katika mkoa wa Kilwa na Yakoma katika mkoa wa Nord-Ubangi. Italazimika kufanya uchaguzi mpya kwenye maeneo hayo.
Hatua nyingine muhimu: Kufuta kura za wagombea 82 wa ubunge na madiwani wa serikali za mitaa .Lakini uchaguzi huo haukufutwa. Hata hivyo matokeo yake hayatazingatia kura za wagombea waliotajwa.
Kisa na maana kulingana na Tume ya Uchaguzi CENI : Kuchochea vurugu na hasa udanganyifu, kumiliki vifaa vya uchaguzi kwa sehemu kubwa ikiwa ni mashini za kura.
Watu waliohusika.
Uamzi huo unawahusu wagombea 36 kutoka majimbo ya uchaguzi 182 ikiwa ni wajumbe kutoka mikoa 17 kwa jumla ya mikoa 26 ya nchi hiyo.
Baadhi ya vigogo wa kisiasa wametajwa kwenye orodha hiyo wakiwemo mawaziri watatu wa Serikali ikiwa ni pamoja na Waziri wa utalii, Waziri wa mafunzo ya kazi, magavana wanne akiwemo Gavana wa Kinshasa lakini pia wakuu wa mashirika ya umma, maseneta na wabunge.
Zaidi ya vyama 30 au muungano wa vyama wamehusishwa na sakata hiyo ya kubatilishwa kwa matokeo hayo wakiwemo sehemu kubwa wagombea kutoka Muungano uliopo madarakani wa 'Union Sacree' unaovishirikisha vyama 12 ikiwemo chama cha UDPS cha Rais Tshisekedi.
Wagombea wengi waliotuhumiwa kwa wizi wa kura au vurugu wamezungumzia kwenye mitandao ya kijamii.
'Ishara ya uhalali wa kura'
Baadhi yao wametangaza nia yao ya kufungua kesi mahakamani. Hata hivyo ni vyama vichache husika vimetoa tamko. Chama cha UNC cha Naibu Waziri Mkuu Vital Kamerhe ambacho wajumbe wake watatu walifutwa kimetangaza kukubaliana na maamuzi hayo.
Kwa upande wa Upinzani, wanahisi kwamba hatua hiyo inakuja kuwapa sheria kwamba uchaguzi haukuwa wa halali
''Sio tu kuchukua hatua kwa uchaguzi wa wabunge na serikali za mitaa lakini hali hii yaashiria kwamba tuna haki pale tunapotilia mashaka kuhusu uhalali wa kura na kupinga matokeo '' alinadi Martin Fayulu.
Mwishoe kuhusu mashirika ya kiraia. Shirika la ACAJ , asasi inayojihusisha na maswala ya sheria limepongeza '' hatua ya busara '' ya Tume ya Uchaguzi CENI kwa kuitaja orodha ya wagombea hao waliofutwa kwenye mchakato wa uchaguzi kuwa ni ''orodha ya aibu''.