Vikosi vya Umoja wa Mataifa nchini DRC, maarufu MONUSCO vimefunga rasmi operesheni yao eneo la Lubero, Kivu Kaskazini, mashariki mwa DRC, baada ya kudumisha usalama eneo hilo kwa miaka 21.
Kufungwa kwa kambi ya Lubero ni katika mchakato mzima wa kufungwa kwa kambi za vikosi vilizoanzishwa tangu 2021, kutokana na tathmini ya pamoja ya hali hiyo kutoka kwa MONUSCO na washirika wake nchini DRC.
Josiah Obat, mkuu wa ofisi ya MONUSCO Beni-Lubero, amesema: "Ujumbe utasalia Beni na, kutoka eneo hili, tutaendelea kushirikiana na washirika ambao tutaondoka hapa. Mbali na hayo, Mashirika ya Umoja wa Mataifa yataendelea kuhudumu na idadi ya watu huko Lubero.’’
Hata hivyo, MONUSCO itasalia nchini DRC kubaki hadi 20 Desemba 2024 ikiwa na majukumu muhimu ya msingi yakiwemo kulinda raia, kusaidia uimarishaji wa sekta ya usalama, na michakato ya kusaidia katika udhibiti wa silaha.
MONUSCO imejisifia kuwa katika kipindi hicho cha miaka 21, imechangia pakubwa utulivu wa mkoa huo ikiwemo kulinda raia dhidi ya vitisho kutoka kwa vikundi vyenye silaha na kusaidia miradi kadhaa kwa niaba ya amani licha ya changamoto tofauti kama vile uwepo wa zaidi ya makundi 40 yenye silaha katika eneo la Lubero pekee.