Na Tuğrul Oğuzhan Yılmaz
Baadhi ya vidonda haviponi, vinaendelea kutoa harufu mbaya na kuongeza maumivu kama vile uchungu wa maovu ya zamani.
Hali hii ni dhahiri nchini Chad, ambapo makovu ya utawala wa kikoloni ya Ufaransa, bado yapo kwenye kumbukumbu ya kizazi ambacho kiliishi katika kipindi cha moja ya maovu mabaya kuwahi kufanyika- wakati wa ukatili wa wa Coupe-Coupe Novemba 15, 1917, katika mji wa Abéché.
"Chad ni yetu, Ufaransa iondoke!" Wito huu wa hasira unajitokeza maeneo yote ya taifa hili la Afrika ya Kati, ikidhihirisha kuongezeka kwa maoni ya watu ambayo yamesbabisha kupungua kuwepo kwa vikosi vya Ufaransa barani Afrika katika miaka ya hivi karibuni.
Tarehe 29 Novemba, wizara ya mambo ya nje ya Chad ilitangaza kufuta makubaliano ya sekta ya usalama na ulinzi kati yao na Ufaransa, wakati ambao Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa alikuwa anazuru nchi yao kwa mkutano na Rais Mahamat Idriss Déby Into siku moja kabla.
Kama ilivyotarajiwa Ufaransa ilijibu kwa tahadhari kuhusu kuvunjwa kwa mkataba huo wa tarehe 5 Septemba, 2019, huku Chad ikisisitiza haki yake ya kimsingi kama taifa huru.
Muda mfupi baadaye, maandamano yakaanza kote nchini dhidi ya kuwepo kwa wanajeshi wa Ufaransa nchini humo.
Kuanzia Disemba 5, maandamano hayo yakaenea hadi katika miji mikubwa, ikiwemo, N'Djamena and Abéché.
Siku kumi kabla ya hapo,mawaidha ya swala Ijumaa katika mjii wa Abéché yaliashiria hatua muhimu ya kuwepo kwa hisia kali dhidi ya Ufaransa katika barabara za Chad.
Tarehe 6 Disemba, raia wa Chad ambao walikuwa wamekusanyika kwa ajili ya swala walianza tena kutafakari juu ya maovu yaliyofanywa na Ufaransa katika eneo lao miaka 107 iliyopita.
Ukatili huu wa Coupe-Coupe ulikuwa vipi kwa historia ya umwagikaji damu kwa Chad kutoka kwa ukoloni wa Ufaransa, na una maana gani kwa watu wake?
Mwandishi wa habari Kamal Koulamallah kutoka shirika la habari la Chad Le N'djam Post ameeleza ukatili wa 1917 mjini Abéché, mji mkuu wa Wadai, kama "doa lisilofutika katika historia ya Chad".
"Unyama dhidi ya watu ambao daima utabaki katika kumbukumbu za watu wa eneo hilo. Kuwadhania watu bila ushahidi, kuwanyanyasa na sera za kikoloni, kipindi hiki kibaya cha ukoloni wa Ufaransa nchini Chad kimebaki katika kumbukumbu za watu kwa karne nzima, hata kwa kukaa kimya, ishara ya kukosa haki na maumivu ," anaeleza.
Wakoloni wakatili
Ufaransa iliendeleza ukoloni wake barani Afrika katika karne ya 19, huku Chad ikiwa moja ya nchi ambazo walilenga kutawala.
Kuanzia mwishoni mwa miaka ya 1800, nchi hiyo iligawanywa kati ya upande wa Uingereza na Ufaransa.
"Kabla ya ukoloni wa mataifa ya magharibi kuja katika bara hili, kulikuwa na utawala wa masultani watatu nchini Chad: Wadai, Bagirmi, na Kanem.
Kwa miaka mingi mataifa haya yalipigana vikali na Ufaransa na walikuwa na uhusiano mzuri na dola ya Ottoman.
Uhusiano huu ulikuwa sawa na kama ulivyo sasa kati ya Uturuki na Chad," Dokta Isa Gökgedik, mhadhiri wa Theolojia katika Chuo Kikuu cha Kütahya Dumlupınar, nchini Uturuki, ameiambia TRT Afrika.
Ufaransa iliingia Chad 1899, na kuanzisha utawala katika mji wa N'Djamena, wakiuita "Fort-Lamy".
Kisha wakataka kupanua utawala wao wa kikoloni katika maeneo ya Abéché, Wadai, Borkou, na Ennedi.
Mwanzo wa 1905, wakakabiliwa na upinzani kutoka kwa vikosi vya Waarabu, Tuareg, Uled Sliman na Sanussi waliokuwa na makao yao Libya na kuungwa mkono na dola ya Ottoman.
Baada ya mapigano ya muongo mmoja, vikosi vya Ufaransa vikiongozwa na Kanali Moll na Dokta Chaopen wakauteka mji wa Abéché tarehe 23 Agosti, 1909.
Katika kipindi hiki, Wadai Sultan Mohammed Salih (Dud Murra) na Dar Masalit Sultan Tajuddin wakaanzisha mapambano.
Makabila kama Abu Sharib, Havalis, Kelingen, Kodoy, Mimi, Veled Cema na Maba, pamoja na vikosi vinavyoungwa mkono na dola ya Ottoman, Sanussi, vikajiunga katika vita, vikikataa utawala wa Ufaransa.
Kanali Moll aliuwawa vitani, pia Sultan Tajuddin aliuawa. Sultan Muhammad Salih na mpwa wake Tajuddin, Bahruddin, waliendelea na mapambano kwa muda lakini wakalazimika kujisalimisha tarehe 27,Oktoba 1911.
Kanali Victor-Emmanuel Largeau aliteka maeneo ya Ain Galaka, Bilma, na Biltine kati ya 1912 na 1914.
Baada ya vita hivi, kukawa na ukame na magonjwa, yaliyosababisha vya watu 322,000 katika mji wa Abéché pekee.
Idadi ya watu ilipungua kutoka 728,000 hadi 406,000 katika kipindi cha miaka mitatu.
Mauaji ya halaiki
Idadi hii kubwa ya watu inaonyesha ukatili uliofanywa kwa watu wa Chad na Ufaransa.
Wakati wa vita vya kwanza vya dunia, maelfu ya watu wa Afrika walichukuliwa kwa lazima wajiunge na jeshi wakiahidiwa watapata uhuru na kupelekwa kufa vitani katika ardhi ya Ulaya wakipambana na Ujerumani.
Licha ya vita hivyo, Ufaransa ilipambana kuweka utawala kamili nchini Chad.
Ili kupunguza makali ya waliokuwa wanapinga utawala wao, walibuni mbinu mahsusi ya kuwaua kikatili viongozi wa kidini waliokuwa wakiheshimika katika jamii.
Bila aibu Ufaransa iliwahadaa viongozi wa jamii na kuwaalika mjini Abéché 1917 kwa madai kuwa walitaka kushauriana nao kuhusu masuala ya utawala bora.
Baada ya swala ya alfajiri, mamia ya wanazuoni wa Kiislamu walivamiwa na kuuawa. Mauaji kama hayo ya kikatili yalifanyika maeneo ya Varya na Kanim.
Mauaji ya kikatili ya Coupe-Coupe au "Kata-Kata" haikuwa tu utekelezaji wa uovu uliopita mipaka kwa wanajeshi wa Ufaransa, ambao walikata vichwa wa wanazuoni wa Kiislamu wa Chad kwa kutumia mapanga.
Vikosi vya kikoloni pia vilichukua vitabu na maandishi ya kihistoria kutoka maktaba, na kuvichoma, au kuvipeleka katika makumbusho nchini Ufaransa, au kuficha chini ya ardhi.
Urithi muhimu wa utamaduni ulifutwa kwa ukatili huo.
Yahya Ould Germa, ambaye alipinga kulazimishwa kujiunga na jeshi, alifungwa jela. Akid Magine na mkewe, Meram Koise, walishinikizwa sana.
Akid Mahamat Dokom, ambaye alikataa kushirikiana na Ufaransa, aliuawa pamoja na mamia ya watu waliokuwa wanamuunga mkono.
Abud Sharara, kiongozi wa kabila la Mehamid, alikamatwa pamoja na watu 40 waliokuwa wakimuunga mkono na kuuawa.
Ili kukabiliana na uwezekano wa mapambano zaidi, wakolono walichukuwa wanajeshi waliokuwa wamepelekwa bara Ulaya kupigana Chad, na kuweka sheria kali za usalama.
Pia walilenga maadili ya kidini ya watu kwa kuwadharau pamoja na kuwakandamiza.
Msikiti mkubwa ulivunjwa, na maandamano katika maeneo ya Salamet na Batha yalizimwa kwa kutumia nguvu kubwa.
Katika kipindi hiki, watu wengi walikamatwa, wengine kuondolewa nchini, na mauaji ya mmoja baada ya mwingine yaliendelea.
Hata mtu akitoa hisia zake kidogo, alikabiliwa kwa mauaji ya kikatili kimya kimya.
Licha ya hayo yote, watu wa Chad hawakukubali utawala wa kikoloni, na waliendelea na upinzani hadi katika miaka ya 1930.
Baada ya miongo ya udhalimu, Chad ikapata uhuru kutoka kwa Ufaransa tarehe 11, Agosti, 1960.
Kulipwa fidia
Ukatili wa Coupe-Coupe bado ni suala nyeti kwa watu wa Chad hadi leo.
Kibaya zaidi ni kuwa Wafaransa bado hawajaomba radhi kwa yale waliyoyafanya kwa eneo hilo na watu wake.
"Baadhi ya wasomi wanataka kuwasilisha kesi katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu dhidi ya Ufaransa, jambo linalokupa taswira kuhusu chuki iliyoko unapotaja kuhusu mauaji ya eneo la Wadai. Kumekuwa na mikutano, na vijana wengi wanafahamu ukatili uliofanyika ," Dokta Mahamat Adoum Doutoum, mhadhiri wa historia katika Chuo Kikuu cha Cheikh Adam Barka mjini Abéché, ameiambia TRT Afrika.
"Idadi ya waliouawa katika ukatili wa Coupe-Coupe Massacre inakadiriwa kuwa 150. Zaidi ya idadi hiyo, ukatili na nia ya mashambulio hayo inaongeza hisia za haki kutopatikana."
Wanazuoni waliouawa na Ufaransa walizikwa katika makaburi ya pamoja katika eneo la Umm Kamil mjini Abéché.
Makaburi hayo yamekuwa sehemu ya kumbukumbu kwa mashahidi, ishara ya mapambano ya watu wa Chad katika kupigania uhuru dhidi ya wakoloni.
"Ukatili wa Coupe-Coupe ni suala linaloibua hisia kali na kuhamasisha raia wa Chad dhidi ya Ufaransa.
Ni jambo linalowaleta pamoja watu, na kutafakari ukoloni kama ulivyokuwa au kuunga mkono uamuzi wa serikali kujiondoa katika makubaliano ya masuala ya ushirikiano wa usalama na ulinzi na Ufaransa," anaeleza Dokta Doutoum.
"Ni wachache tu ambao hawajaonyesha kuunga mkono uamuzi wa serikali. Licha ya kuwa kimya, hilo halijatatiza hamasa kubwa iliyopo kwa watu katika kuunga mkono uamuzi huo."
Katika kuwakumbuka waliouawa katika ukatili wa Coupe-Coupe Massacre mwezi mmoja uliopita, Raia wa Chad kote nchini waliapa kutosahau yaliyofanywa na Ufaransa kwa nchi na watu wao. "Ufaransa iondoke!" – sauti yao ikipaa zaidi hasa katika kipindi hiki.
Pata habari zaidi kupitia Whatsapp channels