Burkina Faso imekuwa timu ya kwanza kufuzu kwa AFCON 2025. Picha: wengine

Burkina Faso imekuwa timu ya kwanza kufuzu kwa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2025, ikiungana na wenyeji Morocco katika michuano hiyo yenye timu 24 kufuatia ushindi wa mabao 2-0 nchini Burundi Jumapili.

Bao la Mohamed Konate na mkwaju wa penalti wa Bertrand Traore, liliifikisha Burkinabe hao hadi pointi 10 kutokana na michezo minne ya Kundi L na kuhakikisha kwamba hawatamaliza nje ya nafasi mbili za juu.

Senegal wako katika nafasi ya pili wakiwa na alama saba kutokana na mechi tatu na pia watafuzu iwapo watashinda ugenini dhidi ya Malawi siku ya Jumanne. Burundi ina pointi tatu katika michezo minne na Malawi haina hata alama moja kwa mechi tatu ilizocheza.

Timu mbili za juu katika makundi 12 ya kufuzu zitatinga hatua ya fainali itakayochezwa kuanzia Desemba 21 mwaka ujao hadi Januari 18, 2026, wakiwa kwenye Kundi B la Morocco ambapo timu nyingine moja itafuzu.

Gabon, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Lesotho ni timu nyingine katika sehemu hiyo.

TRT Afrika