Tangu ilipochukua madaraka, serikali kuu ya Burkina Faso imejitenga na Ufaransa na kuegemea Urusi.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Burkina Faso imethibitisha kupitia taarifa kuwa, "Urusi ilifungua rasmi ubalozi wake Alhamisi hii mjini Ouagadougou."
Uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili ulioanza 1967, lakini Urusi ilifunga ubalozi wake nchini humo mwaka 1992, nayo Burkina Faso ikachukua hatua kama hiyo mwaka 1996 kwa kufunga ujumbe wake jijini Moscow.
Ubalozi wa Urusi ulihamishwa kutoka Ouagadougou hadi Abidjan nchini Ivory Coast, taifa jirani lililoko Afrika Magharibi.
Ubalozi wa Urusi ulifunguliwa katika sherehe iliyohudhuriwa na Waziri Mkuu wa Burkina Faso Apollinaire Joachim Kyelem de Tambela, Waziri wa Mambo ya Nje Karamoko Jean Marie Traore, maafisa wengine wa serikali, na Balozi wa Urusi nchini Ivory Coast Alexei Saltikov, ambaye alisifu urafiki na uhusiano kati ya nchi hizo mbili na serikali hizo.
Balozi wa Urusi nchini Ivory Coast, Alexei Saltykov, amesema kuwa ataongoza ujumbe huo wa Burkina Faso hadi pale balozi mpya atakapotangazwa na kutaja Burkina Faso kama mshirika wa zamani ambaye wana uhusiano thabiti na wa kirafiki.
"Licha ya kutokuwepo kwetu hapa, ushirikiano kati ya nchi hizi zetu mbili katika nyanja za kisiasa na kiuchumi haujakoma," alisema.
Balozi huyo ameongeza kuwa Urusi itaendelea kuisaidia nchi hiyo katika kukabiliana na ugaidi kwa kutoa mafunzo ya usalama na kijeshi.
Mnamo Oktoba, Burkina Faso ilisaini makubaliano na Urusi kwa ajili ya ujenzi wa mtambo wa nyuklia ili kuongeza usambazaji wa nishati kwa nchi ya Sahel ambapo chini ya robo ya idadi ya watu pekee ndio wanapata umeme.
Ushirikiano kati ya nchi hizo mbili utatoa fursa zaidi kwa maendeleo na utatumika kama kichocheo cha ushirikiano wenye ufanisi, Waziri wa Mambo ya Nje Burkina Faso, Traore alisema katika hafla hiyo.