Kamati ya wajumbe 10 ya Ukaguzi na Hesabu za Serikali (CAPA) ya Bunge la Afrika (PAP) leo, inaanza ziara ya siku mbili ya Bunge la Afrika Mashariki (EALA) mjini Arusha, Tanzania ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha muundo wake na kuboresha utekelezaji wa majukumu yake.
Kulingana na taarifa iliyotolewa na Afisa Habari Mwandamizi wa EALA, Nicodemus Ajak Bior ziara hiyo inalenga kupata uzoefu wa kuendesha shughuli zake kutoka kwa wabunge wa Afrika Mashariki.
Kupitia ziara hiyo, CAPA imeazimia kulinganisha, kuchambua na kupendekeza uanzishwaji wa Bunge madhubuti la Afrika. Ziara hiyo pia imelenga kuangazia maeneo muhimu kama vile udhibiti wa ndani, uadilifu, usimamizi wa fedha na rasilimali watu.
Kamati hiyo pia itatumia fursa ya namna hiyo kutathmini muundo wa PAP wa sasa na kuainisha maeneo ya kuboresha.
"Ziara hiyo itawapa CAPA fursa ya kuchota uzoefu kutoka EALA, ikiwa ni pamoja na kuchunguza miundo na kazi za kamati, michakato ya kuajiri na kufanya maamuzi pamoja na kuboresha mawasiliano," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Wabunge hao, pia watapata fursa ya kukutana na Spika wa EALA, Joseph Ntakirutimana.