Botswana inafanya uchaguzi mkuu / picha: AFP 

Uchaguzi mkuu unafanyika nchini Botswana huku rais wa sasa Mokgweetsi Masisi, mwenye umri ya miaka 63 akigombea muhula wake wa pili na wa mwisho.

Amepeperusha bendera ya Chama cha Demokrasia cha Botswana yani Botswana Democracy Party ambacho kimetawala taifa hilo la kusini mwa Afrika kwa miaka 58, tangu uhuru kutoka kwa Uingereza mwaka 1966.

Wagombea wengine ni Duma Boko mwenye miaka 51 anayeongoza Muungano wa Vyama vya Upinzani chini ya chama cha Umbrella for Democratic Change (UDC).

Rais wa sasa wa Botswana Mokgweetsi Masisi, mwenye umri ya miaka 63 anagombea muhula wake wa pili na wa mwisho/ picha: Reuters 

Dumelang Saleshando mwenye miaka 53 anagombea urais chini ya chama cha Botswana Congress Party (BCP).

Naye Mephato Reatile ni kiongozi wa chama cha Botswana Patriotic Front, mojawapo ya vyama vipya vilivyo na wabunge wanne pekee bungeni.

Wapiga kura wapatao milioni 1 watachagua wabunge 61 wa Bunge la Kitaifa na viti 609 vya udiwani katika serikali 16 za mitaa kote nchini.

Chama chenye viti vingi ndicho kitamchagua rais.

Nchi ya fahari asili

Nchi hii ya Afrika Kusini yenye takribani watu 2.7 milioni ina sifa kubwa sana duniani kwa madini yake hasa almasi.

Botswana ni ya pili kwa uzalishaji wa almasi, baada ya Urusi, huku vito vikubwa vilivyopatikana katika muongo mmoja uliopita vikitoka nchini humo.

Agosti 2024 almasi ya pili kwa ukubwa kuwahi kupatikana ya karati 2,492 ilifukuliwa katika moja ya migodi ya nchi hiyo.

Botswana ni ya pili kwa uzalishaji wa almasi, baada ya Urusi Picha: Reuters 

Botswana pia inatambulika kwa idadi kubwa ya tembo ambao serikali inasema ni zaidi ya 130,000.

Hata hivyo serikali imesema idadi hiyo ni tishio kwa wananchi. Aprili 2024, Rais wa Botswana anayegombea muhula wa pili sasa, alitishia kupeleka tembo 20,000 Ujerumani baada ya Wizara ya Mazingira ya Ujerumani kupendekeza kuwe na vikwazo vikali vya kuagiza vitu kutoka kwa wanyama wa kuwinda.

Mwezi Machi 2024 Waziri wa Wanyamapori wa Botswana alitishia kutuma tembo 10,000 katika Hifadhi ya Hyde ya London ili Waingereza "wapate ladha ya kuishi pamoja" nao.

Botswana ina zaidi ya tembo 130,000 ambao wamekuwa changamoto kwa raia/ Picha: AP

Botswana iling'aa katika Michezo ya Olimpiki ya Paris ya 2024 baada ya mwanariadha wake Letsile Tebogo kunyakuwa dhahabu katika ubingwa wa mita 200 kwa wanaume.

Na huku nchi hii ikienda katika uchaguzi, changamoto za kiuchumi, ukosefu wa ajira ni kati ya changamoto ambazo wagombea urais wanaahidi kuzipatia utatuzi.

TRT World