Bingwa wa dunia wa mbio za marathon, Mkenya Kelvin Kiptum, amefariki kufuatia ajali ya barabarani katika barabara ya Eldoret-Kaptagat, mkoa wa Bonde la ufa.
Kiptum, 24, na kocha wake raia wa Rwanda Gervais Hakizimana walifariki papo hapo walipopata ajali mbaya mwendo wa saa 11 usiku Jumapili huku mtu wa tatu aliyekuwa kwenye gari lao dogo akipelekwa hospitalini.
Haya yanajiri chini ya wiki moja tu baada ya Wanariadha wa Dunia kuidhinisha rekodi yake ya dunia ya mbio za marathon.
Kifo cha Kelvin Kiptum kimeishtua nchi nzima ya Kenya na dunia nzima hasa katika ulimwengu wa riadha huku wengi wakizungumzia ndoto kuvunjika na nyota wa bingwa mwenye matumaini makubwa kuzima mapema sana.
''Tumeshtushwa na kuhuzunishwa sana kujua kuhusu msiba wa Kelvin Kiptum na kocha wake, Gervais Hakizimana,'' alisema rais wa shirikisho la raidha duniani Sebastian Coe.
Sebastian Coe alimsifia Kiptum kama 'Mwanariadha wa ajabu akiacha urithi wa ajabu, tutamkosa sana.'
Viongozi wa ngazi za juu serikalini wakiongozwa na Waziri Mkuu Musalia Mudavadi walielezea mshtuko wao mkubwa kufuatia taarifa ya kifo cha mwanariadha huyo chipukizi.
Bingwa wa Olimpiki anayeshikilia Rekodi ya Dunia ya mita 800 David Rudisha pia alielezea huzuni yake kufuatia kifo cha Kiptum.
“Nimeshtushwa na kuhuzunishwa sana kujua kifo cha Kelvin Kiptum na kocha wake Gervais Hakizimana. Rambirambi zangu kwa familia, marafiki, udugu wa riadha na Kenya kwa ujumla. Hii ni hasara kubwa,” alisema Rudisha.
Shirikisho la riadha Kenya, pia imechapisha rambi rambi zake katika mtandao wa X, ''Rambirambi zetu zinakwenda kwa familia zao na jumuiya nzima ya riadha katika kipindi hiki kigumu.'' chapisho hilo lilisema.
Kiptum alikuwa mwanamume wa kwanza kuwahi kukimbia marathon chini ya 2:01 alipokimbia 2:00:35 na kushinda Chicago Marathon Oktoba mwaka jana.
Rekodi yake ya Dunia imeidhinishwa wiki jana na Shirikisho la Riadha Duniani IAAF.
Pia alikuwa ametajwa katika timu ya Kenya kwa Michezo ya Olimpiki huko Paris 2004 na alipangwa kuungana na mtangulizi wake wa rekodi ya dunia Eliud Kipchoge.