Benki Kuu ya Uganda (BoU) imetoa angalizo la uwepo wa mfumuko wa bei utakaotokana na mivutano ya kisiasa inayoendelea ulimwenguni.
Taasisi hiyo ya fedha inasema kuwa mivutano ya kisiasa inayoendelea ulimwenguni itapaisha bei za nishati na gharama za usafirishaji na hivyo kuibua mfumuko wa bei nchini humo.
Licha ya kupungua kwa mfumuko wa bei, BoU inaonya kuwa maendeleo hayo yanaweza kushusha thamani ya sarafu ya nchi hiyo.
Tayari, Benki Kuu ya nchi hiyo imepunguza riba yake kutoka asilimia 10 hadi 9.75 ili kuleta mabadiliko katika mwenendo wa ukopaji katika taasisi za fedha, ambao kwa sasa uko zaidi ya asilimia 18.
Akitoa mwelekeo wa uchumi wa nchi hiyo kwa mwezi Oktoba, Naibu Gavana wa BoU, Dkt Michael Atingi-Ego alisema kuwa tathmini iliyofanywa, ilionesha kuwa mfumuko wa bei utakuwa chini ya asilimia 5, kulingana na mabadiliko na maendeleo yanayoendelea hivi sasa ulimwenguni.
“Ni vyema kurahisisha sera yetu ya fedha ili kukabiliana na mfumuko wa bei,” alisema Naibu Gavana huyo.