Rais Paul Kagame ni babu kwa wajukuu wawili na amejaliwa watoto 4. Picha: Paul Kagame

Rais wa Rwanda Paul Kagame amekuwa akionyesha upendo kwa wajukuu wake wawili, tangu kuwa babu 'rasmi' baada ya binti yake wa pekee, Ange Kagame, na mumewe Bertrand Ndengeyingoma, kujaaliwa mtoto Julai 19, 2020.

Tangu alipopata taji la 'babu', rais wa Rwanda Paul Kagame ameonekana kujawa na furaha na kuchapisha mapenzi yake kwa wajukuu wake wawili mara kwa mara.

Safari ya furaha ya Rais Kagame na mkewe Jeannette Kagame, ilianza pale bintiye Ange Kagame, na mumewe Bertrand Ndengeyingoma, walipofunga ndoa Julai 2019.

Rais Kagame na Wajukuu. Picha: X - Paul Kagame

Mwaka mmoja baadaye, Ange na Bertrand walijaaliwa mtoto wao wa kwanza, Anaya Abe Ndengeyingoma, tarehe 19 Julai 2020 na kuwa mjukuu wa kwanza wa rais Kagame.

Ingawa Paul Kagame pia alihudumu kama mwenyekiti wa AU kutoka 2018 hadi 2019 na kuongoza Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka 2018-2021, wadhfa wa 'babu', ndio anaonekana kupendelea zaidi.

Punde tu alipobarikiwa mjukuu wake wa kwanza, Rais Kagame aliandika, "Tangu jana tumejawa furaha sana na sisi na 'rasmi' babu, na nyanya. Hongera A&B!!

Wajukuu hao wawili wamezaliwa tarehe sawa ingawa walizaliwa miaka miwili tofauti.

Kagame amekuwa akionyesha upendo wake kwa wajukuu kutumia mtandao wa X mara kwa mara.

"Ninaketi na wasichana wangu kwa ajili ya siku yao ya kuzaliwa. Siku sawa 19 Julai!!! LUV," aliandika.

Rais Kagame alijaaliwa mjukuu wake wa pili, Amalia Agwize Ndengeyingoma aliyezaliwa mnamo tarehe 19 Julai 2022.

Pia akiwa kazini, hachelei kuonyesha mapenzi yake kwa wajukuu wake.

"Rafiki yangu mdogo alisisitiza kuja kunitembelea mahali pangu pa kazi na kunikumbusha kwenda nyumbani na kupumzika! Anapendeza," aliandika kwenye mtandao wa X.

Rais Kagame na mama Jeannette Kagame wamejaliwa watoto wanne, Ange Kagame, Ivan Kagame, Brian Kagame, na Ian Kagame.

Rais Kagame na familia yake. Picha: Paul Kagame

Kwa wakati mmoja, Rais Kagame ameonekana akimtania Mkurugenzi mkuu wa shirika la Afya Duniani WHO Tedros Adhanom, ambaye pia alionyesha furaha kwa kuwa babu kwa mara ya kwanza.

"Hongera Dr. Tedros. Mimi niko mbele yako, kwa muda tu. Kila la kheri kwa wazazi na mwanao!! " Rais Kagame alimuandikia Tedros.

Rwanda iliweka historia Julai mwaka huu, kwa kuwa nchi ya Kwanza ya Afrika kuwa mwenyeji wa 'Mkutano wa 'Women Deliver Conference', mkutano mkubwa zaidi duniani juu ya usawa wa kijinsia na afya, haki, na ustawi wa wasichana na wanawake katika karne ya 21.

"Tunasherehekea hadhi, usawa na haki ya fursa ya kila mwanamke. Heri njema ya siku ya wanawake duniani kwa kina mama zetu, dada na binti." Rais Kagame aliandika.

Mbali na kufurahia kuwa babu, rais Kagame pia hutumia majukwaa yake kuangazia masuala binafsi ya familia ikiwemo kuwakumbuka wazazi wake. "Najua mama ni mtu spesheli kwa wengi. Mama yangu pia alikuwa mtu maalum sana kwangu. Ametuacha. Mungu ampumzishe kwa amani." Aliandika.

TRT Afrika