Mahamat, kwenye taarifa kupitia jukwaa la mtandao wa kijamii la X, alisema kwamba alikaribisha uamuzi wa wanachama wa G20 kwa maridhio makubwa.
Taarifa yake inajiri baada ya mataifa wanachama wa G20 kuipa AU hadhi ya mwanachama wa kudumu.
Aidha, amebainisha kuwa wamekuwa wakitetea uanachama kamili wa AU katika G20 kwa muda mrefu.
"Uanachama huu, ambao tumekuwa tukiutetea kwa muda, utatoa mchango mkubwa katika ulinzi wa bara hili na kukabiliana na changamoto za kimataifa." Mahamat alisema.
Wakati huo huo, rais wa Kenya, William Ruto naye ameungana na mwenyekiti wa AU kukaribisha ushirikishwaji wa umoja wa Afrika AU katika muungano wa G20.
''Kenya inakaribisha uanachama mpya wa Umoja wa Afrika G20,'' alisema Rais Ruto. ''Afrika ni bara linalokua kwa kasi zaidi duniani kwenye G20. Hatua Hii itaongeza sauti ya Afrika, mwonekano, na ushawishi katika jukwaa la kimataifa na kutoa jukwaa la kuendeleza maslahi ya pamoja ya watu wetu,'' aliongezea.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo katika mji mkuu wa New Delhi, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi, alisema, "Ninamwalika mwakilishi wa Umoja wa Afrika kuchukua nafasi yake kama mwanachama wa kudumu wa G20." alisema.