Maelfu ya Maafisa wa polisi wa kike kutoka Afrika wenye vyeo mbalimbali, wemekongamana mjini Dar es Salaam nchini Tanzania kwa mkutano wa Jumuiya ya Askari Polisi wa Kike Duniani (IAWP) Ukanda wa Afrika.
Kulingana na msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania Kamishna Msaidizi Mwandamizi David Misime, mkutano huo wa kihistoria barani, unaolenga kuboresha uhusiano na utendaji baina ya askari wa kike, umewaleta pamoja wakuu wa polisi na maafisa wa vitengo mbalimbali ili kujadili usimamizi bora na utekelezaji sheria, kupeana mawazo na kushauriana juu ya uzoefu wa kiutendaji, kuchangiana fikra na kubadilishana taarifa za kiintelijensia, na warsha za mafunzo kwa askari hao.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania, IGP Camillus Wambura amewapongeza Askari Polisi wa kike wanaoshiriki katika mkutano huo utakaoendelea hadi mwisho wa wiki ijayo, huku ukijumuisha mafunzo mbalimbali kuboresha utendaji kazi wa maafisa hao.
Tanzania ambao ndio wenyeji wa mkutano huo, wanawakilishwa na maafisa wa vyeo mbalimbali kutoka vitengo kama vile Jeshi la Polisi Tanzania, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Jeshi la Magereza, Jeshi la Uhamiaji, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mahakama, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Wengine ni pamoja na wawakilishi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Mamlaka ya Wanyamapori (TAWA), Waendesha Mashtaka, Wanasheria wa Serikali, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Wasimamizi wa Sheria na Wadau mbalimbali, na Watumishi raia wa Jeshi la Polisi Tanzania pamoja na wake wa Askari wa Jeshi la Polisi Tanzania.
Jumuiya ya Askari Polisi wa Kike Duniani ni shirika la kimataifa la maafisa wa polisi wa kike na wanawake wanaoshikilia majukumu mengine yanayohusiana na haki ya jinai.