Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza kwenye Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF) unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam tarehe 07 Septemba, 2023.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan hii leo ameshiriki Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula, AGRF, barani Afrika ambapo amepata wasaa wa kujibu maswali ya vijana kuhusu mazingira yanayowekwa na serikali yake ili kuwawezesha kufanya kilimo chenye tija na kuwavutia wengi zaidi kushiriki shughuli za kilimo.

Kuhusu namna gani serikali yake inasaidia kupata masoko kwa ajili ya mazao ya kilimo, Rais Samia amesema hivi serikali inataka kuhakikisha wakulima wanakutanishwa na wanunuzi moja kwa moja bila kuwa na mtu wa kati ambaye amekua sababu ya mkulima kuuza mazao kwa bei ya chini.

Baadhi ya viongozi wa mataifa ya Afrika leo wanashiriki Mkutano huo wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Barani Afrika unaoendelea jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Wakati huo huo, rais Samia ameongeza kusema kuwa serikali inaendelea kuwekeza katika mazingira yatakayowezesha shughuli za kilimo kufanyika kwa ufanisi huku akitolea mfano uwepo wa miradi ya ujenzi wa miundombinu kama vile barabara, reli ya kisasa na kuongeza ufanisi wa bandari akisema yote yanalenga kuimarisha mnyororo wa thamani katika kilimo.

Kama chachu ya kuhimiza na kutoa hamasa kwa vijana katika kilimo, zawadi kwa vijana washindi wa tuzo za miradi bora ya kilimo zimetolewa kwa vijana wawili. Hasima Andriatsitohaina kutoka Madagascar na Ikena Nzewi kutoka Nchini Nigeria.

Marais wastaafu nao ni miongoni mwa washiriki wa mkutano huu unaowakutanisha washiriki zaidi ya elfu nne kutoka mataifa mbalimbali duniani. Rais Mstaafu wa Tanzania Jakaya Kikwete na Goodluck Jonathan wa Nigeria ni miongoni mwa viongozi hao ambapo wameeleza namna walivyosaidia sekta ya chakula wakati wa uongozi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza kwenye mjadala wa masuala ya Kilimo na Vijana wakati wa Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF) unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam tarehe 07 Septemba, 2023.

Tafiti zinaonyesha, zaidi ya asilimia 75 ya fursa za ajira nchini Tanzania inatokana na sekta ya kilimo.

Baadhi ya viongozi wa mataifa ya Afrika leo wanashiriki Mkutano huo wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Barani Afrika unaoendelea jijini Dar es Salaam, Tanzania.

TRT Afrika