Biden / Photo: AP

Rais wa Marekani Joe Biden alisema Jumatatu kwamba anakusudia kusitisha ushiriki wa Gabon, Niger, Uganda na Jamhuri ya Afrika ya Kati katika mpango wa biashara wa Sheria ya Ukuaji na Fursa Afrika (AGOA).

Pia alitoa mfano wa Niger na Gabon kushindwa kuanzisha au kufanya maendeleo endelevu kuelekea ulinzi wa vyama vingi vya kisiasa na utawala wa sheria.

"Licha ya mazungumzo ya kina kati ya Marekani na Jamhuri ya Afrika ya Kati, Gabon, Niger na Uganda, nchi hizi zimeshindwa kushughulikia wasiwasi wa Marekani kuhusu kutofuata vigezo vya kustahiki vya AGOA," Biden alisema katika barua kwa spika wa Baraza la Wawakilishi la U.S.

Biden alisema ataendelea kukagua utendaji wa nchi hizo.

Visingizio vya Marekani

Hatua hii ya Marekani haishangazi kwani tayari ilishaanza kuchukua hatua zingine awali kufuatia mabadiliko ya utawala katika nchi hizo au kukosa kubadilisha sera kwa maslahi ya Marekani.

Mwezi Uliopita Marekani ilitangaza kusitisha misaada kwa taifa la Gabon ikitaja ukosefu wa demokrasia na kufanywa kwa mapinduzi ya kijeshi nchini humo.

Upande wa Uganda tayari kumekuwa na vuta nikuvute kati ya Marekani na serikali ya Museveni, kufuatia sheria waliopitisha ya adhabu kwa wapenzi wa jinsia moja.

Maneno makali yamebadilishwa kati yao ikiwemo kutishia Marekani kuwa itasitisha ufadhili wa sekta ya afya, na elimu ambazo imekuwa ikichangia.

Misaada inayokuja na masharti

Wadadisi hata hivyo wanasema kuwa Marekani imekuwa ikitumia misaada yake katika mataifa haya kusukuma ajenda za magharibi ambazo zinaonekana kukataliwa na mataifa mengi ya Afrika.

Hata hivyo licha ya vitisho hivi, pia kuna hoja kuwa Marekani inachukua hatua kwa makini kwani haitaki kuachia ushawishi wake ndani ya Afrika.

Tayari nchi za Afrika zinaonekana kusogeana karibu zaidi na nchi nyingine tajiri kama vile China na Urusi, na kadri Marekani inavyoendelea kuvuruga uhusiano wake na nchi za Afrika, ndivyo ushawishi wa China na Urusi unavyoongezeka barani.

Licha ya vitisho vya awali, mataifa kama Uganda, Mali na hata Gabon wameshikilia msimamo wao na kukataa kuruhusu misaada yenye masharti.

Kwa mujibu wa shirika la Reuters, Biden anakusudia kusitisha uteuzi wa nchi hizi kama nchi zinazofaidika kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara chini ya AGOA, kuanzia Januari 1, 2024.

AGOA ni mpango wa biashara kati ya Marekani na baadhi ya mataifa kusini mwa jangwa la Sahara, unaowezesha kufutwa kwa kodi kwa bidhaa zinaozwa.

Mpango huo ulianzishwa mwaka 2000, kwa lengo la kuinua uchumi wa nchi hizo kupitia biashara.

TRT Afrika na mashirika ya habari