Afrika Kusini imeanzisha Kamati ya Kuratibu Maafa huko Western Cape baada ya kuonya kuhusu uwezekano wa mafuriko makubwa na yenye hatari katika jimbo hilo siku ya Jumatatu.
Idara ya Huduma ya Hali ya Hewa ya Afrika Kusini ilitoa onyo la uwepo wa dhoruba ya kiwango cha tisa hali iliyopelekea kufungwa kwa shule siku ya Jumatatu.
Wafanyakazi wa kudhibiti majanga wamewekwa katika hali ya tahadhari, mamlaka inasema, huku pepo kali zikisababisha maafa katika jimbo lote mwishoni mwa juma, na kuangusha paa na miti.
Barabara nyingi ndani ya makazi ya watu katika manispaa ya Moqhaka zimefurika maji kutokana na mvua kubwa za mawe zilizokumba maeneo ya Kroonstad na Maokeng, Shirika la Habari la SABC limeripoti.
Msemaji kutoka manispaa ya Moqhaka Dika Kheswa ameviambia vyombo vya habari kuwa ni mapema kwa manispaa hiyo kujua athari za mvua hizo.
Wakazi wametakiwa kuepuka maeneo ya mabondeni na karibu na madaraja.
Mamlaka ziliongeza kuwa upepo mkali unachochea takriban moto 40 katika jimbo lote, moja ambayo imeteketeza takriban vibanda 300, na takriban watu 2,000 tayari wameathirika.