Athari za mvua katika eneo hilo/ Picha: Getty  / Photo: Getty Images

Mamlaka katika jimbo la Eastern Cape imetuma timu za waokoaji kufuatia mvua kubwa zilizoikumba eneo hilo.

Watu saba wamethibitishwa kufa na wengine zadi ya 2,000 kukosa makazi baada ya maeneo ya ghuba ya Nelson Mandela na mji wa Buffalo kukumbwa na mvua.

Msemaji wa serikali katika eneo hilo Khuselwa Rantjie amewataka wananchi wa eneo hilo kuwa waangalifu wakati mafuriko hayo yakiendelea.

"Serikali inawataka wananchi kuwa waangalifu zaidi , hasa katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko, na kufuata taarifa za mara kwa mara na maonyo kutoka kwa Huduma za Hali ya Hewa za Afrika Kusini," Rantjie alisema katika taarifa yake.

Bwawa kupasuka

Mjumbe wa baraza la eneo lilioathirika zaidi, Zolile Williams, amesema kuna hofu ya kupasuka kwa bwawa katika eneo la Kariega.

Wakati huohuo, idara ya hali ya hewa ya Afrika Kusini imetoa tahadhari ya kiwango cha nne kwa eneo la pwani ya kusini ya KwaZulu-Natal.

Mamlaka zinasema timu za majanga ziko katika hali ya utayari katika maeneo ambayo huenda yakaathiriwa.

Msemaji wa Manispaa ya eThekwini, Gugu Sisilana, anasema utabiri unaonesha kuwa mvua kubwa zinazoendelea kunyesha zinaweza kusababisha mafuriko ya barabara na makazi, uharibifu wa miundombinu, kulingana na shirika la habari la Utangazaji la Afrika Kusini (SABC).

Tahadhari ya kiwango cha 4

"Mfano wa utabiri unaonyesha mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika KwaZulu-Natal, ikiwa ni pamoja na eneo la eThekwini. Onyo hili la Kiwango cha 4 linaweza kusababisha mafuriko ya barabara na makazi, uharibifu wa miundombinu na uharibifu wa nyumba zilizojengwa kwa udongo.

"Mvua nyingi zinazoendelea kunyesha zinatarajiwa katika maeneo ya pwani ya eThekwini. Utabiri unaonyesha uwezekano mkubwa wa kunyesha kwa wastani hadi juu kati ya saa sita mchana leo na saa 11 jioni,” alisema Sisilana.

TRT Afrika