Afrika Kusini itapeleka maafisa wa kijeshi wapatao 2,828 kutoa usalama wakati wa uchaguzi mkuu wa Mei 29.
Rais wa nchi hiyo, Cyril Ramaphosa, alisema Jumanne kwamba maafisa wa kijeshi wataongeza nguvu kwa huduma ya kitaifa ya polisi katika kudumisha sheria na utaratibu.
Upelekaji maalum wa maafisa wa kijeshi wakati wa kipindi cha uchaguzi, ambao umepangwa kwa bajeti ya rand milioni 59.5 ($3.3 milioni), utaendelea hadi Juni 7.
Ofisi ya rais wa Afrika Kusini ulisema katika taarifa kwamba Ramaphosa alikuwa amewaarifu kaimu spika wa Bunge la Taifa na mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mikoa kuhusu kupeleka jeshi katika maeneo mbali mbali.
Chama tawala kina hatari ya kupoteza wingi wa viti
Karibu wapiga kura milioni 28 wataenda kupiga kura Jumatano kuchagua viongozi wapya, wakiwemo wabunge, ambao watapiga kura kumchagua rais katika kipindi cha wiki mbili zijazo.
Kwa mara ya kwanza katika historia, chama tawala cha Afrika Kusini, African National Congress (ANC), kinatazamia uwezekano wa kushindwa kupata angalau asilimia 50 ya kura zinazohitajika ili kiweze kuunda serikali peke yake.
Iwapo ANC itashindwa kupata wingi wa viti bungeni, huenda kitahitajika kuingia katika makubaliano ya muungano na vyama vingine vyenye idadi kubwa ya wabunge.
Mbali na ANC, vyama vingine vikuu vya kisiasa nchini Afrika Kusini ni Democratic Alliance (DA), Economic Freedom Fighters (EFF), na chama kipya cha uMkhonto weSizwe (MK), kinachoongozwa na Rais wa zamani Jacob Zuma, ambaye amezuiwa kugombea katika uchaguzi ujao.
Ukosefu wa ajira
Bunge la Taifa la Afrika Kusini lina wanachama 400. Ili mgombea wa urais kushinda katika duru ya kwanza ya upigaji kura, angalau wabunge 201 lazima wapige kura kwa ajili yake.
Tume ya uchaguzi ya Afrika Kusini imeidhinisha wagombea karibu 14,900 kugombea viti 887, ikiwa ni pamoja na nafasi za mabunge ya majimbo.
Karibu asilimia 25 ya watu wazima waliwaambia mtandao wa utafiti wa pana-Afrika Afrobarometer kwamba wanataka serikali itakayounda ajira.
Masuala mengine ambayo wapiga kura wanataka yashughulikiwe ni pamoja na kutatua tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara, kupunguza pengo la tabaka, kukabiliana na uhalifu, na kupambana na ufisadi.