Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Barani Afrika (Africa CDC) kimeipongeza Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa kuzindua chanjo ya ugonjwa wa ugonjwa Mpox nchini humo.
Ujio wa dozi zipatazo 265,000 nchini humo, ni hatua muhimu kwa DRC kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo, kituo hicho kimesema.
“Africa CDC kinaipongeza DRC kwa hatua hiyo muhimu yenye kuashiria nguvu ya uongozi katika sekta ya afya hususani kwa kutilia mkazo watu walio katika mazingira hatarishi," amesema Dkt Jean Kaseya, Mkurugenzi Mkuu wa Africa CDC.
Kulingana na Dkt Kaseya, kituo chake kitaendelea kufanya kazi kwa karibu na DRC ili kuhakikisha kuwa chanjo hizo zinawafikia wahitaji kwa wakati muafaka ili kuzuia milipuko mingine.
"Kipaumbele chetu ni kutoa chanjo zenye ufanisi zaidi," alieleza.
Mpox ni ugonjwa wa virusi unaopatikana kwa Wanyama (Nyani), kutokana na shughuli za kibinadamu. Hutoka kwa wanyama na kuhamia kwa binadamu na kupelekea kuambukizana kutoka kwa binadamu mmoja hadi mwingine.