FRELIMO imekuwa madarakani tangu Msumbiji ilipopata uhuru kutoka kwa Ureno mwaka 1975. / Picha: Reuters

Takriban watu 10 wameuawa nchini Msumbiji katika maandamano ya kupinga uchaguzi wa urais wa Oktoba 9, ambao ulimwendea mgombea wa chama cha FRELIMO Daniel Chapo.

Shirika huru la Kituo cha Uadilifu wa Umma nchini humo (CIP), linasema vifo hivyo vimerekodiwa katika maeneo tofauti ya nchi kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi, zilizotokana na maandamano yaliyoongozwa na vijana.

Mji mkuu wa Msumbiji Maputo ulikumbwa na kiasi kikubwa zaidi cha maandamano hayo baada ya Chapo kutangazwa mshindi kwa karibu asilimia 71 ya kura siku ya Alhamisi.

FRELIMO imekuwa madarakani tangu Msumbiji ilipopata uhuru kutoka kwa Ureno mwaka 1975.

Ofisi za chama cha FRELIMO zachomwa moto

Mgombea huru Venancio Mondlane, anayeungwa mkono na Watu Wenye Matumaini kwa Maendeleo ya Msumbiji (PODEMOS), aliibuka wa pili kwa 20% ya kura.

Mgombea mkuu wa upinzani, Ossufo Momade, wa chama cha RENAMO aliibuka wa tatu kwa karibu 6% ya kura.

Vyombo vya habari vya Msumbiji vinaripoti kuwa ofisi tatu za chama tawala cha FRELIMO zilichomwa moto na waandamanaji, huku maduka kadhaa yakiporwa na magari kuchomwa moto.

Mamia wamekamatwa, huku takwimu rasmi za polisi zikionyesha kuwa 20 wamepata majeraha katika maandamano hayo.

Rais ahimiza utulivu

Polisi pia wanasema kuwa maafisa wasiopungua wanane wamejeruhiwa katika maandamano hayo, na kwamba washukiwa 44 wamefunguliwa kesi za uhalifu dhidi yao.

Polisi walilazimika kurusha vitoa machozi ili kuvunja maandamano hayo ambayo yametokana na madai ya udanganyifu katika uchaguzi wa chama tawala. RENAMO imetoa wito wa kubatilishwa kwa matokeo ya uchaguzi.

Maafisa wa kutekeleza sheria nchini Msumbiji bado hawajatoa takwimu rasmi za vifo, lakini vyombo kadhaa vya habari nchini Msumbiji vinaripoti kuwa kuna vifo katika maandamano yanayoendelea.

Rais anayemaliza muda wake wa Msumbiji Filipe Nyusi, ambaye amemaliza mihula miwili, amewataka raia kuwa watulivu mbele na baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi.

TRT Afrika