Kiongozi wa upinzani nchini Israel, Avigdor Lieberman, alitoa wito wa kufunguliwa kwa uchunguzi wa jinai dhidi ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo Benjamin Netanyahu kwa tuhuma za uhaini. Lieberman anamtuhumu Netanyahu kwa kujaribu kuiIngiza Israel katika vita dhidi ya Iran ili kuepuka kushindwa katika Uchaguzi Mkuu unaofanyika Jumanne ya 27 Oktoba, 2026.
Lieberman, ambaye anaongoza chama cha mrengo wa kulia cha Yisrael Beiteinu, aliwasilisha ombi rasmi kwa Mwanasheria Mkuu wa Israel, Gali Baharav-Miara, kwa mujibu wa taarifa ya shirika la utangazaji la Israel, KAN.
Katika barua yake, Lieberman alisema kuwa kwa muda wa mwezi mmoja uliopita, Netanyahu amekuwa akiwashinikiza maafisa wakuu wa usalama kuchukua hatua zinazoweza kusababisha makabiliano ya kijeshi na Iran.
“Katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amekuwa akiwashinikiza viongozi wa vyombo vya usalama kuchukua hatua zinazoweza kusababisha hali ya kufanya maamuzi yasiyo sahihi kuhusu Iran, na hivyo kuibua makabiliano,” Lieberman aliandika.
Alimtuhumu Netanyahu kwa kujaribu kuishirikisha Israel katika vita vingine kutokana na hofu ya kushindwa katika uchaguzi.
“Kujaribu kuingiza Taifa la Israel katika vita usiku wa kuamkia uchaguzi, pamoja na utayari wa kutoa maisha ya wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) kama kafara kwa sababu tu ya hofu ya kushindwa katika uchaguzi, ni uhaini dhidi ya taifa, usalama wake na wanajeshi wa IDF,” alisema Lieberman.
Aliongeza: “Ninataka uchunguzi wa jinai ufunguliwe mara moja dhidi ya Benjamin Netanyahu kwa tuhuma za uhaini.”
Mapema Jumatatu, Lieberman alitoa tuhuma kama hizo wakati wa mahojiano na kituo cha redio cha Israel cha 103FM, kwa mujibu wa gazeti la Israel la Maariv.
“Netanyahu analisaliti waziwazi taifa anapotaka kutuingiza katika vita,” Lieberman alisema, huku akimtuhumu waziri mkuu kuwa tayari kuhatarisha maisha ya wanajeshi kutokana na hofu ya kushindwa katika uchaguzi.
Mvutano wa kisiasa na wa kijeshi
Kiongozi huyo wa upinzani pia alidai kuwepo kwa mvutano ambao haujawahi kushuhudiwa kati ya uongozi wa kisiasa na ule wa kijeshi wa Israel.
"Hakujawahi kuwa na mvutano kiasi hiki kati ya uongozi wa kijeshi na ule wa kisiasa kama ilivyo leo," alisema, akihusisha hali hiyo na jitihada za Netanyahu za kuchochea hatua inayoweza kusababisha mtafaruku kuhusuiana na Iran.
Lieberman alisisitiza kuwa hatua yoyote ya kijeshi inayoweza kusababisha vita au makabiliano makubwa, inahitaji kujadiliwa na kuidhinishwa na serikali kwa mujibu wa sheria za Israel.
Pia alimtuhumu Netanyahu kwa kujaribu kudhoofisha uhalali wa Kamati Kuu ya Uchaguzi pamoja na matokeo ya uchaguzi, akionya kuwa jitihada kama hizo zinaweza kusababisha mzozo mkubwa ndani ya Israel.
"Wakati huo huo, tunashuhudia juhudi zilizoongezeka kutoka kwa Netanyahu za kupinga uhalali wa Kamati Kuu ya Uchaguzi na matokeo ya uchaguzi, hata kama itakuwa sababu ya mzozo mkubwa wa ndani, vita vya wenyewe kwa wenyewe, au kusambaratika kwa taifa," alisema.
Lieberman alidai zaidi kuwa Netanyahu alikuwa anafahamu uwezekano wa kushindwa katika uchaguzi huo, na hivyo alikuwa akijaribu kuchochea mvutano zaidi na Iran.
"Hata Netanyahu mwenyewe anajua kuwa atakwenda kushindwa. Ndiyo maana anaonyesha wasiwasi uliopitiliza na kujaribu kutuingiza kwenye vita," alisema.
Hadi sasa Netanyahu hakutoa majibu kuhusiana na tuhuma hizo za Lieberman.
Mvutano wa uchaguzi
Shutuma hizo zilitolewa kabla ya uchaguzi mkuu wa Israel siku ya Jumanne, huku kukiwa na mvutano mkali na Iran.
Siku ya Jumapili, Netanyahu alidai kuwa taarifa za kijasusi za Israel zinaonyesha kuwa Iran na washirika wake katika eneo hilo wanaweza kufanya mashambulizi yenye lengo la kuvuruga uchaguzi huo.
Aliionya Iran dhidi ya vitendo kama hivyo, akitishia kutoa jibu kali la kijeshi.
Tarehe 13 Oktoba, Lieberman alimtuhumu Netanyahu kwa kuandaa uwezekano wa mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran, Hamas, au Hezbollah ili kubaki madarakani, akidai kuwa waziri mkuu huyo anasukumwa na hamu ya kujihakikishia kubake kisiasa badala ya kuzingatia masuala ya usalama.
Aidha, tarehe 18 Oktoba, Netanyahu aliweka wazi sera mpya ya usalama wa taifa, akibainisha kupinduliwa kwa serikali ya Iran kama lengo la kimkakati na kusisitiza umuhimu wa kufanya operesheni za kijeshi za kuzuia tishio kabla halijatokea.
Shutuma hizo za hivi karibuni zinakuja huku kukiwa na mvutano unaoendelea kati ya Israel na Iran, kufuatia makabiliano ya kijeshi yaliyotokea mapema mwaka huu.
















