Winga wa zamani wa Barcelona na Chelsea Pedro amestaafu kucheza soka la kulipwa Jumatano akiwa na umri wa miaka 39, akitundika daluga baada ya miongo zaidi ya miwili.
"Naona kama wakati umefika sasa wa kuangazia mambo mengine katika maisha yangu," Pedro aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa Marekani Instagram.
"Nimefurahi kwa kutimiza ndoto yangu na kwa watu wote ambao wameniunga mkono kutimiza hili. Nashkuru, soka, kwa kunipa furaha."
Pedro alijiunga na kituo cha soka cha Barcelona La Masia mwaka 2004 kabla ya kujihakikishia namba kwenye kikosi cha kwanza na kuwa sehemu ya kipindi cha mafanikio cha historia ya klabu hiyo ya Hispania.
Alishinda mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Barcelona 2009, 2011 na 2015, na kufunga goli wakati wa ushindi wao wa 3-1 dhidi ya Manchester United kwenye fainali ya 2011.
Pedro alikuwepo Barcelona kwa misimu saba kabla ya kujiunga na Chelsea mwaka 2015.
Akiwa England kwa misimu mitano, alishinda Kombe la Ligi Kuu, la FA na Ligi ya Europa na Chelsea.
Alielekea Italia baada ya kuondoka Chelsea mwaka 2020, akichezea timu ya Roma na baadaye kujiunga na mahasimu wao Lazio mwaka 2021.
Pedro aliondoka Lazio baada ya msimu wa 2025-26, akiwa amefunga magoli matano kwa timu hiyo.
Kwa mechi za kimataifa, Pedro alivaa jezi ya timu ya taifa mara 65 na kuifungia Hispania magoli 17, kusaidia nchi yake kushinda Kombe la Dunia 2010 na lile la UEFA Euro 2012.















