Marekani siku ya Jumatano imetoa wito kwa Ethiopia na Eritrea kuchukua hatua za kupunguza mvutano, huku kukiwa na hofu ya kuzuka kwa vita kati ya nchi hizo jirani zilizopo katika eneo la Pembe ya Afrika.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, alisisitiza suala hilo katika mazungumzo ya simu na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi yake, Rubio alisema kuwa nchi zote katika eneo la Pembe ya Afrika zinapaswa kuheshimu mamlaka na uhuru wa mipaka ya nchi jirani, pamoja na kujiepusha na uvamizi unaovuka mipaka ya nchi nyingine.
Katika barua iliyoelekezwa kwa wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wiki hii, Ethiopia ilieleza kuwa vikosi vya Eritrea vimeingia hadi kilomita 60 ndani ya Tigray katika siku za hivi karibuni.
Ethiopia imeonya kuwa itajilinda dhidi ya uwepo wa majeshi katika ardhi yake. Hata hivyo, Eritrea imekana taarifa za kuingia kwa majeshi yake katika eneo hilo.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema kuwa Rubio alisisitiza kwamba eneo hilo haliwezi kuvumilia mzozo mwingine.





















