Kuanzia majengo yanayoteketea na maduka yaliyoporwa nchini Ufaransa, hadi mapambano na polisi wa kutuliza ghasia nchini Italia na Ubelgiji, Ulaya imeshuhudia wikendi ya machafuko yaliyochochewa na hasira dhidi ya kupanda kwa gharama za maisha, elimu, na makazi.
Ufaransa imeibuka kuwa kitovu cha wimbi la hivi karibuni la maandamano.
Kilichoanza na wanafunzi wanaoandamana kupinga mazingira duni ya shule, uhaba wa walimu, na kupanda kwa gharama za elimu, kimegeuka kuwa vuguvugu pana zaidi dhidi ya gharama za maisha na kuzorota kwa huduma za umma.
Siku ya Jumamosi, Oktoba 17, maelfu ya waandamanaji waliingia mitaani kote nchini Ufaransa. Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo ilikadiria idadi ya washiriki kuwa takriban 550,000, huku waandaaji wakitoa makadirio makubwa zaidi.
Mamia ya waandamanaji wakamatwa
Hata hivyo, maandamano hayo hayakuwa ya amani. Maduka yaliporwa, moto uliwashwa, majengo ya umma yaliharibiwa, na waandamanaji walikabiliana na polisi.
Katika mji wa Limoges, jengo la kihistoria la halmashauri ya mji lenye miaka 140 lilichomwa moto, huku miji ya Paris, Marseille, na mingineyo ikishuhudia pia makabiliano na uharibifu.
Mamlaka nchini Ufaransa ziliripoti kukamatwa kwa mamia ya watu wakati wa maandamano ya Jumamosi, huku wengine zaidi wakikamatwa kadiri machafuko hayo yalivyoendelea.
Na Ufaransa haikuwa peke yake.
Ubelgiji, Italia na Ureno pia zilishuhudia maandamano makubwa mwishoni mwa wiki.
Mjini Brussels, polisi walitumia gesi ya machozi na mizinga ya maji huku makabiliano yakiongezeka.
Wimbi la maandamano
Huko Milan na Bologna, waandamanaji walipambana vikali na polisi, huku waandamanaji mjini Lisbon wakiandamana mitaani wakilalamika kuhusu mishahara midogo, gharama za maisha zinazoongezeka na mgogoro wa makazi.
Katika wimbi kubwa la maandamano, nchi sita zimetambuliwa kama maeneo yenye vurugu kali zaidi, Ufaransa, Ubelgiji, Italia, Ureno, Hispania na Albania.
Hata hivyo, maandamano hayo si sehemu ya harakati moja iliyopangwa, na masuala hayo hutofautiana kutoka nchi hadi nchi.
Huko Hispania, hasira imejikita katika nyumba za gharama ya juu , kodi zinazoongezeka na kufukuzwa kwa watu kutoka makazi yao.
Wasiwasi miongoni mwa vijana
Huko Albania, waandamanaji wameibua wasiwasi kuhusu ufisadi, ukosefu wa ajira na viwango vya elimu na hata hisia ya familia ya Trump kununua ardhi huko.
Kwa hivyo, ni nini kinachounganisha maandamano haya?
Shinikizo kwenye bajeti za familia, wasiwasi kuhusu ubora wa huduma za umma, na wasiwasi unaoongezeka miongoni mwa vijana wanaohisi kwamba elimu, ajira na nyumba zinazidi kuwa ngumu kuzifikia.
Machafuko hayo pia yanatoa changamoto ya kisiasa kwa serikali za Ulaya ambazo tayari zinakabiliwa na shinikizo la kiuchumi na kutoridhika kwa umma.
Kwa sasa, swali ni kama serikali zinaweza kushughulikia mambo yanayokatisha wanannchi wao tamaa kabla ya maandamano zaidi kuanza?






















