Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) Gianni Infantino ameeleza nia ya kutoa fedha zaidi kwa mashirikisho kote duniani kutoka kwa akiba yao ya $6 bilioni.
Infantino aliwaambia marais wa mashirikisho ya mabara sita ya FIFA kuwa mapendekezo ya fedha zaidi yatajadiliwa katika mkutano wa Baraza la FIFA wa Oktoba 15.
Rais anasema hatua hiyo inafuatia wito wa Rais wa UEFA Aleksander Ceferin, Rais wa Concacaf Victor Montagliani na Rais wa Shirikisho la Bara Asia Shaikh Salman bin Ebrahim Al Khalifa.
“Sitotaja kiwango,” Infantino alisema.
“Nitaunga mkono ongezeko lolote kubwa la fedha ambalo litafikia mashirikisho kupitia mchakato wa FIFA wa utawala bora, liwe na usawa na kuungwa mkono na mpango wa uwazi na uwajibikaji.”
Ceferin na Montagliani walipendekeza tarehe 18 Septemba kuwa FIFA itoe kiwango cha chini $10 milioni kwa kila shirikisho miongoni mwa mashirikisho yote 211 katika kipindi cha mwaka 2027-30 kutoka kwa akiba yake, kiwango hiki kikiwa tofauti na kile ambacho FIFA inatoa tayari.
Infantino alimuagiza Katibu Mkuu wa FIFA Mattias Grafstrom kuzingatia mapendekezo hayo kwenye mfumo mmoja wakati wa mkutano wa tarehe 15 Oktoba na kuwataka Ceferin, Montagliani na Shaikh Salman kueleza mchakato wa utoaji fedha pamoja na taarifa zaidi kuhusu namna hili litakavyofanyika.
Wiki iliopita, Infantino alisema katika barua kwa wajumbe wa Baraza la FIFA na marais wa mashirikisho yote 211 akieleza nia yake ya kufanya mazungumzo kuhusu mabadiliko katika shirikisho hilo la mpira duniani.
Kwa sasa Infantino ndiyo mgombea pekee wa uchaguzi wa FIFA mwakani, huku tarehe ya mwisho kwa wagombea kuwasilisha nia ikiwekwa Novemba 18.




















