Chuo cha Kiufundi cha Mashariki ya Kati cha Uturuki (METU) kinapanga kupeleka kigari ‘Cheri’ mwezini kufikia 2030, mkuu wa chuo aliiambia Anadolu.
Ahmet Yozgatligil, akizungumza pembeni mwa Mkutano wa 77 wa Kimataifa wa Mambo ya Anga (IAC) uliofanyika mkoa wa kusini magharibi wa Antalya, alieleza kuwa mfano wa kigari hicho cha kuzunguka tayari umeshatengenezwa na kinafanyiwa majaribio.
Mradi wa Cheri unajumuisha vigari viwili vinavyowezeshwa na Akili Mnemba (AI) na kutengenezwa kwa ushirikiano na Shirika la Anga la Taifa la China (CNSA).
Vigari hivyo viwili vimetengenezwa kuhimili baridi kali na vina mwanga mdogo kwa upande wa kusini wa mwezi, vikienda sanjari kufanya tathmini na kutambua sampuli za miamba.
“Vigari vyetu viwili vya kuzunguka vitafanya kazi pamoja na pia kupiga ‘selfie’ vikiwa mwezini, huku vikiwa vinaendeleza shughuli za tathmini katika maeneo yatakayovumbuliwa, jambo ambalo tunafurahia kwa kweli,” alisema.
Mfano wa kigari cha Cheri ulikabidhiwa Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Mkuu wa Baraza la Elimu ya Juu (YOK), Erol Ozvar, wakati wa hafla ya mwaka wa elimu ya kitaifa.
“Wanafunzi wetu zaidi ya 120 wanafanya kazi katika mradi huu pamoja na wahadhiri katika kitivo, ikiwa sehemu ya mpango wa EU wa ‘Go Space’, wanafunzi wetu pia wanaangazia kuimarisha utaratibu wa mawasiliano wa setalaiti angani, na vituo kuanzishwa,” alisema.
Yozgatligil alieleza kuwa kitivo pia kinachangia katika sekta ya anga kupitia miradi kama mpango wa Aselabs kwa kushirikiana na kampuni ya sekta ya ulinzi ya Aselsan.
Alisema Chuo cha METU hivi karibuni kilishirikiana katika utafiti na vyuo vikubwa barani Ulaya na Marekani, baada ya kusaini makubaliano na Axiom Space.
“Mradi muhimu wa kimataifa tunaoshughulikia kwa sasa ni Kituo cha Teknolojia ya Anga cha METU, ambacho kitakuwa eneo la sekta ya utafiti wa anga na biashara,” aliongeza.
Kongamano hilo la masuala ya Anga IAC 2026 lilianza Jumatatu na litaendelea hadi Ijumaa. Wenyeji wake ni Shirika la Anga la Uturuki (TUA) na upande wa sekta ya ulinzi wa SAHA Istanbul pamoja na Wizara ya Viwanda na Teknolojia.



















