| Swahili
ULIMWENGU
5 dk kusoma
Miaka mitatu ya vita vya Gaza: Jinsi Israel ilivyoharibu miundombinu muhimu
Miundombinu iliyoharibiwa, uhaba wa umeme na vikwazo dhidi ya upatikanaji wa bidhaa muhimu vimewaacha wakazi wengi wa Gaza wakihangaika kupata maji salama na huduma za usafi wa mazingira.
Miaka mitatu ya vita vya Gaza: Jinsi Israel ilivyoharibu miundombinu muhimu
Israel imewahamisha kwa nguvu mamia ya maelfu ya Wapalestina katika mauaji ya hakaiki dhidi ya Gaza. / / Anadolu Agency

Katika ukanda wa Gaza, kupata maji ya kutosha kumekuwa changamoto ya kila siku. Familia hubeba ndoo, hupanga foleni kwenye malori ya maji na kulazimika kutenga kiasi kidogo cha maji kwa ajili ya kunywa, kupika na kuoga.

Watoto hutumia saa nyingi kutafuta na kuteka maji badala ya kwenda shule.

“Kabla ya vita, hatukukabiliwa na hali hii,” Hanadi Al Aff, Mpalestina aliyelazimika kuhama makazi yake na anayeishi mji wa Gaza pamoja na watoto wake watano, aliiambia Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) mwezi Juni.

“Tunahifadhi maji na kuyaweka kwa ajili ya mambo muhimu zaidi, ambayo ni kunywa, kupika na kuwaogesha watoto,” alisema.

Miaka mitatu baada ya Israel kuanza vita vyake vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza mwezi Oktoba 2023, mifumo ya maji, usafi wa mazingira na umeme katika eneo hilo bado imeharibiwa kwa kiwango kikubwa. Hali hiyo imewaacha mamilioni ya watu wakitegemea misaada ya dharura na miundombinu inayofanya kazi chini ya uwezo wake.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotajwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) mwezi Septemba, asilimia 91 ya kaya zilikuwa zikikabiliwa na ukosefu wa usalama wa maji.

Karibu theluthi moja ya kaya zilikuwa zinapata maji chini ya viwango vya chini zaidi vinayokubalika katika mazingira ya kibinadamu, huku asilimia 88 zikiripoti matatizo ya kupata huduma salama za usafi wa mazingira.

Uharibifu uliosababishwa na mashambulizi ya Israel katika eneo hilo ni mkubwa. Kwa mujibu wa ripoti nyingine iliyotajwa na Umoja wa Mataifa, asilimia 88 ya miundombinu ya maji, usafi wa mazingira, pamoja na asilimia 76 ya mitandao ya chini ya ardhi, ilikuwa imeharibiwa.

Shirika la Msalaba Mwekundu lilisema uzalishaji wa maji umeshuka hadi takribani asilimia 40 ya kiwango kilichokuwepo kabla ya vita.

Uhaba wa umeme unazidisha mgogoro

Uzalishaji wa maji bado uko katika hatari ya kuvurugika. Kwa mujibu wa ripoti ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, iliyotolewa mwishoni mwa Septemba, kiasi cha maji kilichokuwa kikipitia katika mabomba matatu kutoka Israel kilikuwa chini kwa takribani asilimia 40 ya kiwango kilichokuwa kimekubaliwa.

Kiwanda cha kuondoa chumvi kwenye maji katika eneo la Deir al-Balah pia kilikuwa kikifanya kazi chini ya uwezo wake kutokana na hitilafu katika mfumo wa kusukuma mabaki ya chumvi, pamoja na utegemezi mkubwa wa jenereta.

Uhaba wa umeme unazidisha zaidi matatizo ya huduma za maji na usafi wa mazingira. Takwimu za Umoja wa Mataifa zilizotolewa mwezi Septemba zilionyesha kuwa asilimia 90 ya miundombinu ya nishati, ikiwemo mtandao wa usambazaji umeme na miundombinu yake ilikuwa imeharibiwa.

Jenereta ni muhimu katika kuendesha vituo ambavyo bado vinafanya kazi, lakini nazo zinategemea mafuta ambayo ni machache na magumu kupatikana.

Maji yasiyo salama yaongeza hatari za kiafya

Uhaba wa maji unachochewa na wasiwasi kuhusu ubora wa maji. Mnamo Agosti, zaidi ya asilimia 73 ya sampuli 938 za maji zilizokusanywa kote Gaza hazikufikia viwango vilivyopendekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO )vya klorini, huku asilimia 18 ikionyesha uchafu na vijidudu.

Reinhilde Van De Weerdt, mwakilishi wa WHO nchini Palestina, alisema mwezi Septemba kwamba uchafuzi wa vijidudu ulikuwa umeongezeka kutoka chini ya asilimia 6 mwezi Januari hadi zaidi ya asilimia 18 mwezi Agosti.

Maradhi ya vipindupindu yameongezeka mara mbili katika kipindi hicho.

Hali ya usafi wa mazingira nayo inazidi kuwa mbaya. Asilimia 39 ya kaya zilizofanyiwa tathmini ziliripoti kuwa taka zilikuwa zikijikusanya karibu na maeneo yao ya makazi, huku asilimia 36 zikisema ziliona maji machafu na tope karibu na maeneo yao.

Msongamano mkubwa katika maeneo ya watu waliolazimika kuyahama makazi yao, vyoo visivyo salama na mifumo duni ya kupitisha maji vinaongeza wasiwasi zaidi, hasa wakati msimu wa mvua unapokaribia.

Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) limeripoti kuenea kwa magonjwa yanayohusishwa na hali duni ya maji na usafi wa mazingira, pamoja na msongo wa mawazo miongoni mwa watu wanaojitahidi kudumisha usafi na utu wao katika mazingira magumu.

Magonjwa ya ngozi yalichangia karibu asilimia 18 ya wagonjwa waliohudumiwa katika vituo vya afya vya msingi vya MSF mwaka 2025. Hali duni ya maji na usafi wa mazingira pia imechangia kuenea kwa upele wa ngozi (scabies) na chawa.

Mashirika ya Misaada Yaonya Kuhusu Kunyimwa Mahitaji ya Msingi kwa Makusudi

MSF pia ilisema mwezi Aprili kwamba mamlaka za Israel zimetumia upatikanaji wa maji kama silaha dhidi ya Wapalestina huko Gaza, na kueleza kwamba kunyimwa maji ni sehemu ya mfumo wa adhabu ya pamoja.

Shirika hilo lilitaja uharibifu wa miundombinu, vikwazo dhidi ya upatikanaji wa misaada ya kibinadamu na kuzuiwa au kucheleweshwa kwa bidhaa muhimu.

MSF pia ilisema malori yake ya maji, yaliyokuwa na alama zinazoonyesha wazi kuwa ni ya misaada, pamoja na visima vyake, vilishambuliwa kwa risasi au kuharibiwa.

“Tangu Januari 1, 2026, maombi yote ya MSF ya kuingiza vifaa kupitia mfumo maalumu, ambapo idhini yake huamuliwa na mamlaka za Israel, yamekataliwa,” shirika hilo lilisema.

Mashirika ya kibinadamu yanaendelea kukarabati miundombinu na kutumia vyanzo mbadala vya maji. Hata hivyo, uhaba wa mafuta, jenereta, vipuri, klorini na vifaa vingine muhimu unatishia huduma chache ambazo bado zinaendelea kufanya kazi.

Kwa familia za Gaza, kurejea katika maisha ya kawaida kunamaanisha kurejesha mahitaji ya msingi: maji salama ya kunywa, huduma zinazofanya kazi za usafi wa mazingira na umeme wa uhakika.

Kwa watoto kama wale wa familia ya Al Aff, hilo pia linaweza kumaanisha kuweka chini ndoo za maji na kurejea shuleni.

CHANZO:Anadolu Agency