Waokoaji wametoa miili ya watoto 13 katika mto Ganges nchini India baada ya boti iliyokuwa imebeba abiria kupita uwezo wake kupinduka ilipokuwa ikielekea katika sherehe za kitamaduni, taarifa hiyo imetolewa Jumatano, huku Waziri Mkuu Narendra Modi akielezea “masikitiko yake” kwa msiba huo.
Boti ilipinduka siku ya Jumanne usiku katika wilaya ya Vaishali mashariki mwa jimbo la Bihar, huku wakazi wakiwahi kuwaokoa watu waliokuwa katika boti hiyo kwa kutumia taa za simu kumulika majini.
"Kulikuwa na giza mara ghafla tulisikia watoto wakipiga kelele na kuomba msaada wakati boti ilipozama,” Ravi Yadav, ambae ni kijana katika kijiji hicho aliyekuwa akisaidia katika uokoaji ameiambia AFP.
"Tulifanikiwa kuokoa watoto watatu, kwa kutumia taa za simu na tochi, kwa sababu kulikuwa na giza.”
Ramlakhan Rai mkazi wa kijiji hicho amesema boti lilikuwa "dogo" na "halikuwa katika hali nzuri,” na kuongeza kuwa watu walisongamana katika boti ambalo halikuwa na uwezo wa kubeba idadi kubwa ya watu.
“Familia kadhaa zimepoteza watoto wao,” amesema.
Watu sita waliokolewa, ikiwemo watoto wawili ambao wapo katika hali mahututi.
Daktari Nirmal Kumar, kutoka kituo cha afya cha eneo hilo, amesema watoto wanne na watu wazima wawili wamepelekwa katika hospitali ya wilaya.
"Tumejaribu kuwasaidia, lakini 13 walikuwa tayari wamepoteza maisha,” amesema Dkt. Kumar.
Varsha Singh ambae ni jaji wa wilaya ya Vaishali ameiambia AFP kwamba miili ya watu 13 imepatikana.
Ajali za boti zinatokea mara kwa mara nchini India, mara nyingi zikisababishwa na msongamano mkubwa wa abiria, na kukosekana kwa vifaa vya kutosha vya kuokoa maisha.



















