Umoja wa Afrika unazindua taasisi ya kwanza ya bara hilo ya kutoa daraja la sifa ya mikopo (credit rating agency), hatua inayolenga kuzipa nchi za Afrika njia mbadala ya taasisi tatu kubwa duniani: Moody’s, S&P Global na Fitch.
Taasisi hiyo, inayojulikana kama Africa Credit Rating Agency (AfCRA), inazinduliwa nchini Mauritius baada ya kazi ya karibu muongo mmoja katika mradi huo.
Viongozi wa Afrika waliidhinisha kuanzishwa kwake mwaka 2018.
Umoja wa Afrika unasema AfCRA itatoa tathmini za sifa ya mikopo kwa kuzingatia takwimu, utaalamu na uhalisia wa kiuchumi wa Afrika, huku ikifanya kazi kwa uhuru bila kuingiliwa na serikali. Itatoa daraja kwa serikali zinazokopa, taasisi za kifedha na makampuni binafsi.
Hatua hii inakuja wakati serikali za Afrika zikikabiliwa na gharama kubwa za kukopa na shinikizo linaloongezeka la madeni.
Kulingana na Umoja wa Afrika, gharama za kuhudumia deni la nje la bara hilo ziliongezeka kutoka dola bilioni 61 mwaka 2010 hadi dola bilioni 163 mwaka 2024.
Taasisi hiyo pia inatarajiwa kupanua wigo wa huduma zake: kwa sasa, nchi 23 za Afrika hazina daraja lolote kutoka kwa taasisi tatu kubwa za kimataifa.
Viongozi wa Afrika wamekuwa wakizishutumu mara kwa mara taasisi hizo za kimataifa kwa kudharau au kutothamini ipasavyo matarajio ya kiuchumi ya bara hilo na kushusha daraja la nchi kwa haraka mno wakati wa majanga.
Taasisi hizo zinakanusha madai ya upendeleo wa kimfumo, zikisema zinatumia mbinu zilezile duniani kote.
Hivyo, AfCRA itakabiliwa na mtihani muhimu wa iwapo wawekezaji watachukulia ukadiriaji wake kuwa wa kujitegemea na wa kuaminika, hasa ikiwa tathmini zake zitatofautiana kwa kiasi kikubwa na zile za taasisi tatu za awali.
Umoja wa Afrika (AU) unatarajia kuwa taasisi hiyo mpya itaongeza imani ya wawekezaji, kuimarisha masoko ya mitaji barani Afrika na hatimaye kusaidia nchi kupata masharti bora zaidi ya ukopaji.



















