Mamlaka ya Kudhibiti Nishati nchini Kenya imetangaza kupandisha bei ya petroli kwa asilimia 6 na dizeli kwa asilimia 4.5 kutokana na kuongezeka kwa gharama za uagizaji wa mafuta, hali inayohusishwa na mzozo unaoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati.
Kenya, ambayo hutegemea kwa kiasi kikubwa mafuta kutoka eneo hilo, ni miongoni mwa nchi zilizoathirika.
Katika mabadiliko hayo ya bei, lita moja ya dizeli jijini Nairobi itauzwa kwa shilingi za Kenya 227.76, sawa na Dola 1.75 kutoka shilingi 217.86. Wakati huo huo, bei ya mafuta ya taa imepanda kutoka shilingi 191.38 hadi shilingi 219.87, sawa na Dola 1.69 kwa lita.
Bei hizo mpya zitatumika kuanzia Oktoba 15 hadi Novemba 14, kipindi ambacho mamlaka hiyo inatarajiwa kutangaza viwango vipya vya bei za mafuta.
Katika hatua ya kupunguza athari za ongezeko hilo kwa wananchi, serikali ya Kenya imeongeza muda wa punguzo la kodi (VAT) kwa mafuta, kutoka asilimia 16 hadi asilimia 8, hadi Januari 14, 2027.
Wataalamu wa uchumi wanaonya kuwa kupanda kwa bei za mafuta kunaweza kuongeza gharama katika sekta mbalimbali, zikiwemo usafirishaji, kilimo na ujenzi.
Ongezeko la gharama za usafiri linaweza pia kuathiri bei za bidhaa na huduma, na hivyo kuongeza mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi.




















